MKAZI wa Galagaza, Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Melkisedeck Mrema amenusurika kufa baada ya kutumbukizwa kwenye shimo la choo na watu waliovamia nyumbani kwake na kumteka mtoto na mke wake.
Saa 10 baada ya tukio hilo, mke wake, Johari Bung'ombe alipatikana akiwa katika shimo la choo nyumba ya jirani alipotumbukizwa na watu hao mita chache kutoka nyumbani kwake.
Akisimulia tukio hilo, Mrema alisema Januari 15 majira ya saa 12 asubuhi alitoka nje ya nyumba yake ili kuhudumia kuku, ghafla walitokea watu hao kwa nyuma na kumpiga kichwani.
Alipogeuka aliwaona wakiwa na nondo, panga na kisu na kuamua kupiga kelele kuomba msaada, lakini walimpiga tena na panga wakimtaka kukaa kimya huku wakimsukuma kurudi ndani.
Alisema walimwingiza ndani na kufunga milango kwa funguo na kumtaka atoe fedha alizo nazo jambo ambalo alipingana nao na kuendelea na purukushani na watu hao.
"Wakiwa wameniweka chini ya ulinzi sebuleni kwangu, mke na mwanangu walikuwa chumbani, walivunja mlango na kuwaleta nilipo," alisema.
"Walipoingia chumbani walimshurutisha mke wangu akawapa fedha iliyopo wakanirudia tena kunipiga nionyeshe nilipoweka hela, nilimwambia iliyopo ndio waliyoichukua, lakini hawakunielewa waliendelea kunishurutisha," alisema.
Mrema alisema mbali ya fedha walichukua simu zote zikiwamo anazotolea huduma ya fedha na kumtaka awape nywila (password), ili waangalie miamala wakatoe fedha zilizopo.
"Niliwapa ili niokoe maisha yangu, mwanangu na mke wangu ambaye ni mjamzito. Hata hivyo, haikusaidia walinifunga mikono na miguu wakanitoa nje huku mke na mwanangu wakiwarudisha chumbani."
Mrema alisema walipotokea nje walimpeleka kwenye karo la shimo la choo wakawa wanalazimisha kumwingiza ndani, lakini kutokana na kumfunga mikono ilishindikana.
"Niliwaambia wanifungue mikono ili waniingize, walifanya hivyo na kunisukuma ndani kwa miguu nikadondokea shimoni, wakafunga na kuondoka sikujua walielekea wapi," alisema.
Akiwa ndani ya shimo, Mrema alisema alipata mti ambao aliutumia kugonga juu ya mfuniko huku akipiga kelele kuomba msaada, hata hivyo alitokea mmoja wa wateja wake ambaye alimkosa kwenye simu na kumfuata nyumbani ndipo aliposikia sauti yake na kufunua shimo.
"Kuna mtu nilikua na ahadi naye aliponikosa kwenye simu na dukani sijafungua alikuja nyumbani majira ya saa mbili hivi, aliposikia nagonga kwenye shimo alifunua nikamuomba anisaidie nitoke. Alitoa taarifa kwa mwenyekiti na majirani wakaja na kamba kunitoa," alisema.
Alisema wakati anatolewa kwenye shimo, alitarajia kumkuta mke wake na mtoto wao wa miezi saba wakiwa ndani, lakini alikuta nyumba imefungwa kwa ufunguo na hakukuwa na mtu ndani.
Mrema aliendelea kusimulia kuwa baada ya kumaliza taratibu za kutoa taarifa za polisi na hospitali, walirudi nyumbani na aliwashauri kuzunguka maeneo ya vichaka na nyumba za jirani kuwaangalia mama na mwanawe.
Mita chache kutoka nyumbani kwake alipita kwenye shimo la choo na kusikia sauti ikiomba msaada, alipojaribu kufunua ikashindikana kutokana na mikono yake kukosa nguvu ndipo alipoomba msaada kwa watu waliokuwa karibu na eneo hilo.
"Walikuja wakafunua tulimkuta mke wangu ndani amechoka baada ya kukaa kwa muda mrefu, nje ya shimo pembeni ya ufuniko hawa watekaji waliziba na majani ionekane kama yameota muda mrefu," alisema.
Mrema alisema mke wake ambaye yupo hospitali kwa matibabu alimweleza kwamba watekaji hao baada ya kumwingiza kwenye shimo hilo walisikika wakisema mtoto inabidi wakamchukue asibaki ndani peke yake.
Hadi saa kumi jioni Januari 16, Nipashe ilipotoka nyumbani kwa Mrema hakukuwa na taarifa ya kupatikana kwa mtoto wala gari.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Galagaza, Said Siasa, alisema wanaendelea kutoa ushirikiano kwa familia hiyo kumsaka mtoto pamoja na wahalifu hao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa operesheni ya kuwasaka watu hao inaendelea.
Kamanda Morcase alisema mafanikio ya awali yaliyopatikana ni kumpata mke wa Mrema Januari 15 majira ya saa 11 jioni na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED