Wenje amjia juu Lema akimtuhumu kuhusika njama kumpindua Mbowe

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:53 AM Jan 17 2025
Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ezekia Wenje.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ezekia Wenje.

MWENYEKITI wa Kanda ya Victoria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ezekia Wenje amemjia juu Godbless Lema, akidai ni miongoni mwa makada waliosuka mpango wa kumpindua Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe alipokuwa gerezani.

Amedai kuna baadhi ya wanachama wa chama hicho, wakiongozwa na Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Lema, walianzisha mpango uliopewa jina la ‘Join the Chain’.

Alisema mpango huo ulikuwa na dhumuni la kukusanya fedha za kuwezesha kuitishwa kikao cha Baraza Kuu na Kamati Kuu ya chama hicho kuwashawishi wajumbe kufanya mapinduzi ya kumteua Tundu Lissu kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa na Mch. Peter Msigwa awe Makamu Mwenyekiti wake.

Wenje alidai hayo jana mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari, akisema: "Mnakumbuka mimi, Lema na Lissu tulikimbia nchi, tukiwa huko mafichoni huku nyumbani mambo yakatokea mengi mpaka Mwenyekiti (Mbowe), akakamatwa akafungwa gerezani.

"Mwaka 2022, (Mbowe) akiwa gerezani, marafiki zangu hawa wakashauriana kwamba waanzishe kitu kinaitwa 'Join the Chain' na Mwenyekiti aliyeasisi hiyo 'movement' ni rafiki yangu, Godbless Lema."

Alidai viongozi hao waliamini kuwa Mbowe kukabiliwa na kesi ya ugaidi asingetoka mahabusu gerezani kwa urahisi.

Wenje alidai kuwa baada ya kushirikishwa mpango huo, aliamua kujiweka pembeni, akisisitiza uamuzi wake huo ukawa mwanzo wa matatizo na tofauti za kimtazamo kati yake na viongozi hao waliokuwa wakipanga njama.

"Niliposhirikishwa mambo kama haya, nilikataa uasi na hii ndiyo sababu kubwa ya kuanza kwa ugomvi mkubwa kati yangu na marafiki zangu, mimi nilikataa kuwa mwasi, nikajiondoa kwenye process (mchakato) yote," alidai Wenje.

ZITTO KUFUKUZWA

Kadhalika, Wenje alidai kuwa hata mpango wa kumfukuza uanachama Zitto Kabwe (wakati huo akiwa CHADEMA), uliongozwa na Lema.

"Hivi ninavyovieleza, hata Mbowe anavijua. Kama si uvumilivu, watu wanaopanga kufanya mapinduzi ndani ya chama bila kufuata Katiba, kina Lema, ndiyo watu ambao hawakupaswa kuwa wana-CHADEMA," alidai Wenje ikiwa ni majibu kwa Lema ambaye juzi alisisitiza kuwa kama angekuwa na mamlaka kichama, Wenje asingekuwa mwanachama wao.

Kuhusu yeye kudaiwa kutumwa na Mbowe kugombea nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA kwa madai ya kumwondoa Lissu, Wenje alidai "hayo ni mawazo ya kidikteta" ya kutopenda agombee. 

LEMA KUSUSA

Kadhalika, Wenje alidai anamshangaa Lema kumtishia Mbowe kuwa akishinda tena nafasi ya Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, hatogombea ubunge wa Arusha Mjini.

"Yeye kama hana ushawishi huko Arusha, anaona mambo ni magumu, aseme tu! Hivyo vingine ni visingizio vidogo vidogo. Ukweli ni kwamba Lema angegombea uenyekiti wa chama Kanda ya Kaskazini angeshindwa vibaya sana, alisoma upepo. Kwa hiyo alikula kona mapema," alidai Wenje.

Mwanasiasa huyo pia alisema yeye na wenzake wako upande wa chama na si upande wa Mbowe kama inavyodaiwa.

Wenje alidai kwamba kuna taarifa amezipata kwamba Lema na wanachama wengine wanapanga kuhama chama hicho endapo watashindwa kwenye uchaguzi huo.

Kadhalika, Wenje alimshutumu Lissu kukimbia kuongoza chama hicho wakati Mbowe akiwa gerezani na kwamba alitegemewa awe miongoni mwa mawakili wa kuongoza jopo la utetezi wakati Mbowe yuko gerezani.

Wenje pia alidai kuwa mpaka sasa Mbowe ndiye mgombea anayeungwa mkono zaidi kuliko ilivyo kwa Lissu.

Katika hilo, Wenje alidai kuwa katika kanda tisa ambazo zimefanya uchaguzi wa ndani wa chama mpaka sasa, viongozi wa kanda nane wanamuunga mkono Mbowe.

Pia alidai wenyeviti na makatibu wengi wa mikoa wa chama hicho wanamuunga mkono Mbowe na ndiyo waliokwenda nyumbani kwake kumshawishi agombee tena kuongoza chama hicho.

Uchaguzi wa viongozi wakuu wa CHADEMA umepangwa kufanyika siku nne zijazo katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.