WAKATI Dunia ipo katika mageuzi ya kiteknolojia katika usafiri wa ndege, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), inatekeleza mkakati wa kugeuza Anga la tanzania kuwa salama na kuvutia safari za ndege za kimataifa.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi, amesema serikali kupitia mamlaka hiyo inaendelea kuboresha miundombinu na kusimamia sheria na kanuni ili watu wengi kutumia usafiri a ndege kupitia katika viwanja mbalimbali nchini.
Msangi amesema wanaendelea kufanya maandalizi kwa ajili ya Ukaguzi wa Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) na kwa sasa TCAA inahuisha kanuni za usafiri ili ziendane mabadiliko mapya kulingana na matakwa ya shirika hilo la kimataifa.
Aidha amesema mikakati mingine ni pamoja na kuendelea utoaji mafunzo kwa ajili ya wakaguzi ili kupata weledi na namna bora ya kufanya kaguzi, usimamizi wa uthibiti wa Usafiri wa Anga na kufanya kaguzi za ndani kutathimini uwezo wa kampuni zilizosajiliwa nchini kwa kuzingatia matakwa ya kanuni za Usafiri wa Anga nchini.
“Tunaendelea kusimamia mafunzo endelevu kwa marubani, wahandisi, na watendaji wengine wa Sekta ya Usafiri wa Anga ili tuweze kuongoza katika sekta ya usafirishaji Afrika,” amesema Msangi.
Mkurugenzi Mkuu huyo wa TCAA, ameongeza kuwa wanafanya uwekezaji katika mifumo ya kisasa ya uongozaji wa Ndege na mawasiliano kuhakikisha inaendana na mabadiliko ya kiteknolojia.
Katika kuhakikisha mamlaka hiyo inaaminika kimataifa, alieleza wanashirikiana na nchi jirani na mashirika ya kikanda na kimataifa kwa lengo la kubadilishana uzoefu.
“Tunafurahi kueleza kwamba tunaendelea kuboresha viwanja vya ndege na miundombinu inayohusiana na usafiri huo na inakidhi viwango vya kimataifa,” amesisitiza.
Katika majumuisho ya kamati hiyo, wabunge waliutaka uongozi wa TCAA, kusimamia kikamilifu mikakati hiyo na pamoja na kuhakikisha chuo cha CATC kinajengwa kukamilika haraka ili vijana wa Kitanzania waweze kupata ujuzi na kuitumikia nchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED