MAKAMU wa Rais Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Laetitia Ntagazwa amewataka mawakili kufanya kazi kwa weledi kwa kujitolea na kuacha maslahi ya pesa mbele katika kesi za muhimu zikiwemo za umma kwa Taifa.
Ameyasema hayo Bagamoyo mkoani Pwani katika kufungwa kwa mafunzo ya siku mbili yaliyowakutanisha mawakili 100 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
“Msisite na kuchelewa kusaidia na kushauri wananchi katika shuhuli zote za uchaguzi hata kama hamna malipo, msitangulize fedha mbele katika kuwasaidia watanzania”
Aliwataka wasiwe wanasaidia majiji makubwa pekee ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya pekee kwani hata kwenye wilaya na kata mikoa yote watanzania wana uhitaji wa msaada wa kisheria kwakuwa maisha hayaishi majiji makubwa pekee.
“Jitoleeni katika kuwasaidia Watanzania kwani kufanya hivyo pia utajitengenezea jina kutokana na kujitolea kwako na si kung’ang’aniamaslahipekee” alifafanua
Ntagazwa alisema wanawashukuru THRDC kwa mafunzo hayo ya siku mbili kwa kundi hilo limeweza kuwakumbusha mawakili hao majukumu yao ya kila siku katika utendaji kazi hasa katika kipindi hiki cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuelekea Uchaguzi Mkuu mwakani.
Nae Mratibu Kitaifa THRDC, Onesmo Olengurumwa alisema mafunzo hayo yalikuwa na lengo la kuwajengea uwezo pamoja na kuwakumbusha majukumu yao namna ya kuendesha mashauri ya kimkakati ya masuala ya kiuchaguzi na masuala yenye maslahi kwa umma.
Aidha alisema mwakani wataangalia namna ya kuongea na mahakama na serikali kuona namna ya kuboresha maeneo yanayogusa maslahi ya umma.
“Tunataka kuongezeka kwa mawakili wenye weledi kwa maslahi ya umma watakaobobea katika mchakato mzima wa masuala ya kiuchaguzi kwakuwa kumekuwa na uhaba wa mawakili hao” alisema
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED