WATU wawili wamefariki dunia katika matukio tofauti, likiwamo la mwanamke Marcelina Chigudulu aliyekutwa amefariki dunia chooni katika chumba alimokuwa amepanga na mwenza wake ndani ya nyumba ya kulala wageni 'Maleta Lodge', kijijini Kilosa, nje kidogo ya Mji wa Mbambabay, wilayani Nyasa.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya alisema mwishoni mwa wiki kuwa, Novemba 17 mwaka huu, saa tatu usiku, katika nyumba hiyo ya kulala wageni, Marcelina, aliyekuwa na ujauzito wa miezi mitatu, alikutwa amefariki dunia.
Kamanda Chilya alisema kwamba inadaiwa siku hiyo ya tukio, Marcelina aliingia katika nyumba hiyo akiwa na mpenzi wake, Hassani Kamtande ambaye ni fundi magari, mkazi wa kijiji cha Buluma, wilayani Mbinga. Ilipotimu saa tatu usiku, iligundulika chumba alimokuwa Marcelina, kinawaka moto, kitendo ambacho kilisababisha majirani kufika eneo hilo kusaidia kuzima moto.
Alisema wakati majirani wakiwa wanaendelea na uzimaji moto katika chumba hicho, waligundua kuwamo mwili wa binadamu uliokuwa umelazwa chooni wakati mwenza wa Marcelina akiwa hayumo katika chumba hicho, akidaiwa kukimbia baada ya kufanya mauaji.
Alieleza kuwa baada ya upelelezi wa kina wa tukio hilo, Jeshi la Polisi lilibaini mtuhumiwa alikuwa na wivu wa mapenzi kwa mwenza wake na ndicho kiini cha kumnyonga wakiwa ndani ya chumba hicho cha kulala wageni na kuchoma vitu mbalimbali likiwamo godoro kwa lengo la kupoteza ushahidi.
Kamanda Chilya alisema mtuhumiwa wa tukio hilo, Kamtande ameshakamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi ya kisheria.
Katika tukio lingine, Kamanda wa Chilya alisema ni la Novemba 14 mwaka huu, saa 12 asubuhi, kitongoji cha Mbilo, kijiji cha Kizuka, tarafa ya Muhukuru, wilayani Songea, ambako Ponsiana Kapinga (22), mkazi wa kitongoji hicho, aliuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani na mumewe Martini Hyera baada ya kumnyima tendo la ndoa kwa muda mrefu.
Alisema kuwa wawili hao walionekana alfajiri wakikimbizana huku mtuhumiwa akiwa ameshika mpini wa shoka na baadaye kutekeleza mauaji hayo kisha kumpigia simu shangazi yake Paulina Nchimbi na kumjulisha kuwa amemuua mke wake na akataja sababu za kumuua kuwa alikuwa anamnyima unyumba kwa muda mrefu.
Kamanda Chilya alisema mwili wa Ponsiana umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya mazishi. Mtuhumiwa Hyera baada ya tukio hilo alikimbia na kutokomea kusikojulikana. Msako dhidi yake unaendelea.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED