Hivi ndivyo Stars ilivyofuzu AFCON mara zote nne

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:21 AM Nov 25 2024
Taifa Stars na Guinea
Mtandao
Taifa Stars na Guinea

NOVEMBA 19, mwaka huu, ikiwa ni mwezi mmoja tu kabla ya miaka 63 ya Uhuru, timu ya soka ya Tanzania, Taifa Stars, ilifanikiwa kutinga fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) kwa mara ya nne.

Lilikuwa ni bao la dakika ya 60 lililowekwa wavuni na winga wa Kimataifa, Simon Msuva, anayecheza soka la kulipwa katika Klabu ya Al Talaba ya Iraq.

Ikiwa kwenye Kundi H, Stars ililazimika kuifunga Guinea ili kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

Hii ni mara ya nne kwa Tanzania kuweza kufuzu fainali hizo tangu ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Waingereza, Desemba 9, 1961.

Kombe la Mataifa ya Afrika ndiyo michuano mama ya kimataifa katika Bara la Afrika, inayosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Ilianza kucheza kwa mara ya kwanza mwaka 1957. Kuanzia mwaka 1968 ilianza kuchezwa mara moja kila baada ya miaka miwili.

Mataifa matatu ndiyo yaliyoanza kucheza michuano hiyo ambayo ni Misri, Sudan na Ethiopia, huku Afrika Kusini ambao walikuwa nao wanataka kushiriki, walizuiwa kutokana na sera za ubaguzi wa rangi wakati huo. Baada ya hapo ikaitwa michuano ya Mataifa Huru barani Afrika, ili kuzuia nchi za Afrika ambazo hazijawa huru na zinazotawaliwa kimabavu, zisitie mguu.

Kwa maana hiyo zikawa zinashiriki timu za Afrika zilizopata uhuru, na zilicheza kwa mtindo wa mtoano na baadaye kupata timu nane ambazo zilikuwa zinacheza fainali zake kwa kuzigawa makundi mawili, A na B.

Fainali hizo zikaitwa Fainali za Mataifa Huru barani Afrika. Na mfumo huo ulichezwa baada ya nchi kadhaa kupata uhuru na kuongeza idadi ya timu.

Kwa sasa nchi zote za Afrika zimepata uhuru na mfumo wa kupata washindi wanaoingia kwenye fainali hizo umebadilika, ikijulikana sasa kama michuano ya AFCON.

Katika makala haya, tunaiangazia safari ya Tanzania ilipokuwa ikitinga fainali hizo kwa mara zote nne.

1. Tanzania 2-1 Zambia (1979)

Stars ilianzia raundi ya kwanza dhidi ya Mauritius, ambapo katika mchezo wa kwanza ugenini Mauritius, Aprili 16, 1979, ilichapwa mabao 3-2, kabla ya kupindua meza nyumbani kwa kuinyuka nchi hiyo mabao 4-0 nchini, Aprili 29, 1979.

Ilikuwa Agosti 11, 1979 jijini Dar es Salaam, Stars iliposhinda bao 1-0 dhidi ya Zambia kwenye mchezo ya raundi ya pili lililowekwa wavuni na Mohamed Rishard 'Adolf', huku mchezo wa marudiano, Ndola Zambia, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, Alex Chola aliwapatia wenyeji bao dakika ya 43, kisha Peter Tino kusawazisha dakika sita kabla ya mechi kumalizika.

Matokeo ya jumla ya mabao 2-1, yaliifanya Stars kufuzu fainali hizo ambazo zilichezwa 1980, nchini Nigeria.

Kwenye fainali hizo, Stars ilishika nafasi ya mwisho kwa kucheza mechi tatu, ilipoteza mbili na sare moja, ikiwa Kundi A pamoja na timu za Ivory Coast, Misri na wenyeji Nigeria wakifuzu. Nigeria ndiyo waliokuwa mabingwa mwaka huo baada ya kuifunga Algeria mabao 3-0 katika mchezo wa fainali.

2# Tanzania 3-0 Uganda (2019)

Tanzania ilifuzu kwa mara ya pili 2019 ilipoifunga Uganda, The Cranes mabao 3-0, mechi ikichezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Machi 24.

Ilikuwa ni miaka 40, baada ya kufuzu mara ya kwanza 1979 nchini Zambia, fainali zake zikichezwa 1980 nchini Nigeria.

Yalikuwa ni mabao ya Msuva dakika ya 21, Erasto Nyoni kwa mkwaju wa penalti, dakika ya 51 na Aggrey Morris.

Matokeo hayo yaliifanya Stars kumaliza nafasi ya pili kwa pointi nane, nyuma ya Uganda iliyokuwa na pointi 13 kwenye Kundi L.

Fainali zake zilichezwa Julai nchini Misri, Stars ikiwa Kundi C, ilimaliza ikishika mkia, safari hii haikupata pointi yoyote, ikipoteza mechi zote tatu dhidi ya Kenya, Senegal na Algeria, bingwa kwa mara nyingine akitoka kwenye kundi lake, nayo ni Algeria, iliyoifunga Senegal bao 1-0.

3# Tanzania 0-0 Algeria (2023)

Tanzania ilifuzu kwa mara ya tatu AFCON 2023, ambapo fainali zake zilichezwa nchini Ivory Coast.

Ikiwa Kundi F na timu za Uganda, Niger na Algeria, ilifanikiwa kumaliza nafasi ya pili nyuma ya Algeria iliyokuwa na pointi 16, yenyewe ikimaliza na pointi nane.

Stars ilihitaji sare tu dhidi ya Algeria na ilifanikiwa kuipata ugenini, Septemba 7, 2023 na kufikisha pointi nane, ikiiacha Uganda na pointi zake saba.

Fainali zake zilichezwa kuanzia Januari 13, mwaka huu, hadi Februari 11, Tanzania ikiwa Kundi F na timu za Morocco, DR Congo na Zambia, kwa mara ya tatu ilishika mkia, lakini safari hii ilipata pointi mbili, ikipoteza moja na sare mbili.

4# Tanzania 1-0 Guinea (2024)

Kwa mara nyingine imepata tena tiketi ya kucheza AFCON mara ya nne. Msuva kwa mara ya pili amehusika kufunga bao la kuipeleka Stars fainali kama ilivyokuwa 2019. Stras haijawahi kushinda mechi yoyote ya fainali za AFCON mara zote tatu ilizocheza. Je, mwakani nchini Morocco kwenye fainali hizo Tanzania itatoka kimasomaso?