Tanzania, Uganda kushirikiana katika miradi ya mafuta na gesi

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 10:05 AM Nov 25 2024
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio.
Picha: Mpigapicha Wetu
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio.

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dk. James Mataragio amesema Tanzania na Uganda zitaendelea kushirikiana katika uendelezaji miradi mbalimbali ya nishati, ikiwamo sekta ya mafuta na gesi.

Dk. Mataragio aliyasema hayo juzi jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kushiriki Jukwaa la Kibiashara kati ya Tanzania na Uganda.

"Tunaangalia ni kwa jinsi gani sekta hii ya mafuta na gesi inaweza ikachangia katika maendeleo ya nchi hizi mbili, tumekuwa na mijadala mbalimbali inayolenga kuendeleza sekta hii ya mafuta na gesi," alisema Dk. Mataragio. 

Aliongeza kuwa, mjadala mkubwa katika jukwaa hilo ni kuangalia namna gani nchi za Tanzania na Uganda zinaweza kushirikiana katika sekta za mafuta na gesi.

Mataragio alisema Tanzania na Uganda zina historia ndefu za ushirikiano, akitolea mfano mradi wa kimkakati wa bomba la kusafirisha mafuta ghafi wa EACOP.

Akielezea mradi huo wa EACOP, Dk. Mataragio alisema umefikia asilimia 47, akisisitiza kuwa kwa sasa uko katika hatua ya kutandaza mabomba. Takribani kilomita 52 za mabomba zimeshachomelewa ambazo zitaanza kufukiwa ardhini.

Akizungumzia faida ya mradi kwa wananchi, alisema Watanzania wamejengewa uwezo katika maeneo mbalimbali na hivi sasa wanafanya kazi kwenye mradi huo.

Kwa upande wa ajira, alisema mradi umetoa zaidi ya ajira 8,000 huku lengo likiwa ajira 10,000.

3