JESHI la Polisi mkoani Ruvuma linawashikilia watu wawili, akiwamo mfanyabiashara wa dawa za mifugo Nickson James (29), mkazi wa mtaa wa Buswelo, Manispaa ya Ilemela, mkoani Mwanza, wakidaiwa kukamatwa wakati wanasafirisha dawa za mifugo zinazodhaniwa ni bandia zenye thamani ya Sh. 78,986,099.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa kutokana na operesheni zinazoendelea katika maeneo yote ya mkoa huo, Novemba 7 mwaka huu, saa 6:30 mchana, huko katika kijiji cha Lilondo, kata ya Wino, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, askari polisi walikamata gari lenye namba za usagili T 185 EBX aina ya Toyota DYNA Truck ambalo lilikuwa linaendeshwa na Frank Ndunguru.
Alidai kuwa gari hilo lilikuwa linatoka Songea kwenda Njombe likiwa limesheheni dawa za mifugo na kwamba mfanyabiashara James aliyekuwa katika gari hilo, ndiye mmiliki wa dawa hizo zilizokamatwa, zikihifadhiwa katika gari lenye kiyoyozi (air conditioner).
Hata hivyo, alidai kuwa ukaguzi wa polisi ulibaini air conditioner hiyo ilikuwa feki.
Kamanda Chilya alifafanua zaidi kuwa baada ya gari hilo kukamatwa, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na timu ya wataalamu wa ukaguzi wa dawa kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) walibaini dawa hizo zimeingizwa nchini kinyume cha sheria kupitia njia za panya na kwamba baadhi ya dawa ni bandia na nyingine zipo chini ya kiwango kwa mchanganuo:
Levimox Super, Alben Blue, Oxysol Plus, Bisol, Piperazine, Tylodoxy200 na Vetoxy 20 kati yake zikiwa chupa 4,044, madumu 1,646 na pakiti 46 zenye thamani ya Sh. 51,174,599; dawa bandia za mifugo aina ya 03 ambazo ni Hi-tet, Levafas Diamond Naoxy-met 10 inj 500ml & 250mlkati yake zikiwa chupa 1,026, madumu 12 zenye thamani ya Sh. 19,456,000; dawa zilizosajiliwa lakini hazina kibali cha kuingia nchini aina ya 03 ambazo ni Ivermed Ascarex na Polytricin kati yake zikiwa chupa 512, pakiti 92 zenye thamani ya Sh. 8,355,500.
Kamanda Chilya alisema upelelezi wa kina juu ya tukio hilo unaendelea kwa kushirikiana na mamlaka husika na jalada la kesi limefikishwa Ofisi ya Mashtaka mkoani Ruvuma kwa hatua zaidi za kisheria.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED