JESHI la Polisi linawashikilia watoto wawili kwa tuhuma za kurusha mawe na kuharibu kwa kuvunja vioo viwili vya treni ya mwendokasi (SGR) katika Kijiji cha Manase, wilayani Chamwino.
Katika taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, DCP David Misime, watoto hao walirusha mawe wakati treni hiyo inapita ikitokea jijini Dar es Salaam kwenda jijini Dodoma Novemba 22, mwaka huu.
Alisema kutokana na hali hiyo, polisi walifanya msako na kuwakamata watoto hao wenye umri wa miaka 16 na 12 (majina tunahifadhi kwa sababu watuhumiwa ni watoto na wanalindwa kisheria), wote wakazi wa kijiji cha Manase wilayani Chamwino.
"Chanzo kilichosababisha uharibifu huo ni baada ya kuona treni ikipita, wakarusha mawe kwa pamoja ili kuona kama mawe waliyorusha yataweza kushindana na mwendo wa treni," alisema.
DCP Misime alitoa wito kwa wananchi wanaoishi maeneo ambamo treni ya kisasa inapita, kuendelea kupeana elimu juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu ya treni kwa maslahi yao na taifa.
"Kila mzazi au mlezi anao wajibu wa kutoa elimu kwa familia, hasa watoto kuacha vitendo ambavyo vitasababisha uharibifu kwa reli na treni ya kisasa kwa kuwa itawasababisha kukinzana na sheria za nchi," alisema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED