CHUO cha Maendeleo ya wananchi Kibaha kinakabiliwa na vikwazo mbalimbali, ukiwamo uhaba wa karakana kwa ajili ya fani za umeme, useremala na ufundi wa ujenzi wa mabomba.
Pia kinahitaji gari la usafiri na usafirishaji huku baadhi ya majengo yakiwa na uhitaji wa ukarabati.
Mkuu wa chuo hicho, Joseph Nchimbi alibainisha hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali yaliyofanyika chuoni huko kwa wahitimu 147 wa fani mbalimbali, akiomba serikali kusaidia fedha za ukarabati na ujenzi wa majengo mapya.
Nchimbi pia aliomba serikali kusaidia fedha za ruzuku kwa ajili ya chakula na uendeshaji wa chuo hicho kama ilivyo kwa vyuo vingine vya FDC vilivyo chini ya Wizara ya Elimu.
Alibainisha kikwazo kingine ni baadhi ya wanachuo kukatisha mafunzo kabla ya kuhitimu muda uliopangwa baada ya kuona wametosheka au kushindwa kumudu gharama za chakula.
"Chuo hiki kinategemea ada, michango ya wazazi kujiendesha hakipati ruzuku ya serikali kwa ajili ya chakula na mahitaji mengine ya uendeshaji kama ilivyo kwa vyuo vingine vya FDC na hivyo kufanya kishindwe kutoa chakula," alisema Nchimbi.
Mkurugenzi wa Elimu Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Dk. Emmanuel Shindika, akizungumza katika mahafali hayo alisema serikali itaendelea kupeleka fedha za ukarabati wa mabweni ya wanachuo na miundombinu mingine, huku akiahidi serikali itaangalia namna ya kutatua changamoto zingine zilizoko.
Alisema serikali imejipambanua katika kuimarisha uchumi kwa kuwa na sera nzuri za kibenki, ukopeshaji na ushirika wa akiba na mikopo na hivyo vijana wanaohitimu wanatakiwa kutumia fursa hizo kwa kujiunga kwenye vikundi na kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na serikali kupitia halmashauri.
Pia aliwataka wahitimu wa chuo hicho kujiunga na vikundi vya uzalishaji mali ambavyo vitakuwa njia ya mafanikio itakayopapatia fursa ya kuunganisha ujuzi na kutumia rasilimali zitakazopatikana katika maeneo yao.
Mkurugenzi wa Shirika la Elimu Kibaha, Robert Shilingi, aliomba serikali kutenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya chuo hicho ili vijana wanaojiunga katika chuo hicho wasome katika mazingira mazuri.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED