Ateba, Mukwala waandaliwa kuiua Bravo do Maquis

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:23 AM Nov 25 2024
KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids
ao
KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amewapa kazi mastraika wake wawili, Leonel Ateba na Steven Mukwala, kuwamaliza Waangola, Bravo do Maquis, katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika, unaotarajiwa kuchezwa keshokutwa, Jumatano katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, kocha huyo raia wa Afrika Kusini, alisema kwa jinsi alivyowaangalia wapinzani wao, anadhani mastraika wake wana uwezo wa kuimaliza mechi hiyo kwa jinsi wanavyocheza.

"Malengo ni kupata ushindi nyumbani, ikiwezekana mkubwa tu, kwa kutumia nafasi tutakazotengeneza zitumiwe kwa usahihi na mastraika wetu ambao tumewapa kazi hiyo tu, kiufundi tayari tumeshawaangalia wapinzani wetu kwenye baadhi ya mechi, hasa ya Ijumaa, Novemba 22, waliyocheza dhidi ya Academica de Lobito kwenye Ligi Kuu nchini Angola," alisema.

Katika mchezo huo, Bravo do Maquis ikiwa ugenini ilitoka suluhu dhidi ya wenyeji wao.

Timu hiyo inashika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu nchini Angola ikiwa na pointi 16, ikicheza michezo 12, ikishinda mitatu, sare saba na kupoteza miwili, ikifunga jumla ya mabao 11, ikiruhusu 10 kwenye wavu wake.

"Mechi dhidi ya Pamba Jiji imetusaidia sana, imewafanya wachezaji wetu wawe kwenye utimamu wa mwili na tayari kwa mchezo huo mgumu, tofauti na tusingecheza, kilichotuathiri kwenye mechi ile ni hali ya uwanja na hali ya hewa, ndiyo maana hatukucheza vema, ila mashabiki wa soka wamiminike kuja kuona soka la kuvutia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa," alisema Fadlu.

Meneja Habari na Mawasiliano wa Klabu hiyo, Ahmed Ally, aliwataka mashabiki wa timu hiyo kuujaza uwanja kama ambavyo wamekuwa wakifanya siku zote na masuala ya ndani ya uwanja wawaachie wachezaji kwani watawalipa kwa ushindi.

"Mnachotakiwa ninyi ni kufika tu ili kuwapa hamasa wachezaji wetu. Pasi na kupepesa macho mechi ya Jumatano ni ngumu, kinachotakiwa ni kwenda kwa wingi ili kuwafanya wageni wajihisi kweli wapo ugenini, wanaweza kufungwa kwa makelele tu ya mashabiki.

"Bravo do Maquis ni timu ngeni na haina uzoefu sana wa mechi za kimataifa, ila ina wachezaji wazuri. Kwa sababu hawajawahi kuona umati wa mashabiki 60,000, siku wakikutana nao utawashangaza, utawatetemesha na kuwa faida kwetu. 

"Kama timu kubwa mfano Al Ahly ya Misri, Wydad Casablanca, Raja Casablanca, Asec Mimosas na nyingine zinajua kasheshe la mashabiki wa Simba wakiwa Benjamin Mkapa," alisema.

Simba ipo Kundi A, na timu za Bravo do Maquis, CS Constantine ya Algeria na CS Sfaxien ya Tunisia.