Olengurumwa aiangukia Tume Haki za Binadamu kumlinda Athumani

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 02:53 PM Jan 15 2025
MRATIBU Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa akizungumza na mkazi wa Kijiji cha Gwata, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, Athuman Mohammed Zuberi.
Picha: Pilly Kigome
MRATIBU Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa akizungumza na mkazi wa Kijiji cha Gwata, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, Athuman Mohammed Zuberi.

MRATIBU Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, ametoa wito kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kuingilia kati kuchunguza sakata la mkazi wa Kijiji cha Gwata, Wilaya ya Kisarawe, Mkoa wa Pwani, anayedaiwa kuondolewa kwa nguvu kwenye nyumba yake na kubomolewa, hali iliyomwacha bila makazi.

Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Wakili Olengurumwa alisema kuwa kinachofanyika kwa Athuman Mohammed Zuberi (46) ni kinyume na haki za binadamu na misingi ya utawala bora. Amesema Zuberi amekuwa akitishiwa maisha na kufunguliwa kesi mbalimbali ili kuachana na madai yake ya nyumba na ardhi.

Kwa mujibu wa taarifa, mwaka 2012, Zuberi alikabidhiwa ardhi ya ekari 20 na viongozi wa kijiji hicho kwa ajili ya kuanzisha makazi. Baadaye aliendeleza eneo hilo na kujenga nyumba ya kudumu. Hata hivyo, kwa sasa anadai kunyanyaswa na kuondolewa kwa nguvu kutoka kwenye eneo hilo.

“Tunaomba hekima, busara, na utu vizingatiwe. Hata kama kuna madai kuwa eneo hilo ni mali ya kijiji, Zuberi alipewa na viongozi wa kijiji kwa ajili ya kujisitiri na familia yake. Tunapendekeza apewe hata nusu ekari ili aweze kuendelea na maisha yake,” alisema Wakili Olengurumwa.

Olengurumwa ameongeza kuwa Zuberi amekuwa akinyanyaswa kwa kubambikiwa kesi, zikiwemo za mauaji, ambazo yeye na mtoto wake walikamatwa na kushtakiwa. Hata hivyo, kwa msaada wa Ofisi ya THRDC, wamefanikiwa kupangua kesi hizo. “Leo mnamuona hapa akiwa huru baada ya juhudi kubwa za kisheria ambazo tumemsaidia bure,” alibainisha.

Wakili huyo alisema tayari amewasiliana na Tume ya Haki za Binadamu ili kushughulikia suala hilo, huku THRDC ikiendelea na juhudi za kukutana na Mkuu wa Wilaya kwa lengo la kuhakikisha Zuberi anapata haki yake.

Kwa upande wake, Athuman Zuberi amekiri kupokea eneo hilo kutoka kwa viongozi wa kijiji na kusema kuwa aliwekeza muda na rasilimali zake kutengeneza makazi ya kudumu. Alieleza kusikitishwa na hali ya sasa, ambapo nyumba yake imevunjwa na hana mahali pa kwenda, hali inayomfanya kuwa katika mateso makubwa.

“Nilikuwa naishi hapo na familia yangu, lakini sasa sina makazi. Hali hii imenikatisha tamaa sana,” alisema Zuberi kwa huzuni.