Meya atishia kujiuzulu kisa tuhuma za rushwa watumishi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:47 AM Jan 15 2025
MEYA wa Halmashauri ya Tabora, Ramadhani Kapela.
Picha:Mtandao
MEYA wa Halmashauri ya Tabora, Ramadhani Kapela.

MEYA wa Halmashauri ya Tabora, Ramadhani Kapela, amesema yuko tayari kujiuzulu iwapo baadhi ya maofisa wa idaya ya ujenzi wa halmashauri hiyo wanaotuhumiwa kula rushwa ya Sh. milioni 20.7 watalindwa na viongozi wa serikali.

Maofisa hao wanatuhumiwa kuhusika na rushwa hiyo ambayo ni ya malipo ya vibali vya ujenzi wa majengo, hivyo kuisababishia manispaa kupoteza mapato.

Kapela alisema hayo kikao cha kupitisha rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 kwa manispaa hiyo ya Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na kumwagiza mkurugenzi wa halmashauri hiyo kushirikiana na vyombo vya dola, kuchukua hatua stahiki. 

Alisema yuko tayari kujiuzulu nafasi yake endapo wahusika hawatachukuliwa hatua za kisheria hata kama wanafahamiana na viongozi wakuu wa serikali, akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan, hivyo anachotaka ni haki kutendeka kwa kuwa watuhumiwa wamekuwa wakifanya hivyo kwa makusudi bila kuogopa.

“Ninaomba niweke wazi kuwa niko tayari kujiuzulu nafasi yangu endapo hawa wahusika hawatachukuliwa hatua za kisheria. Kama watalindwa mimi ninaachia ngazi. Mkurugenzi na vyombo vya dola washughulikieni hawa na mkishindwa mtawajibishwa,” alisema.

Suala hilo limeonekana kuwakwaza madiwani wa manispaa hiyo na kuunga mkono kauli na maagizo ya Mstahiki Meya.

Aidha, Katibu wa CCM Wilaya ya Tabora, Daniel Mhina, alikemea baadhi ya wafanyabiashara na wawekezaji wanaokwepa kulipa kodi na kuanza kuomba msaada kwa njia za panya kutoka kwa viongozi wa chama na serikali.

Mhina alisema inasikitisha kuona watumishi walioaminiwa na serikali wanaingia katika tuhuma za rushwa na kusababisha manispaa kukosa mapato huku wahusika wakijineemesha jambo hilo ambali kwa mujibu wa kiongozi huyo, haliwezi kuvumiliwa.

Siku chache zilizopita, kuliripotiwa kuwapo  na malalamiko kutoka kwa Umoja wa Madereva Mkoa wa Tabora (UWAMATA) wakiwashutumu baadhi ya watumishi wa manispaa hiyo kuchukua pesa kwa watu na kuwaruhusu kujenga vibanda kwenye eneo la kituo cha magari yaendayo Sikonge, Uyui na Urambo, maarufu kama Maduka 30.

Uchunguzi ulibaini kuwapo kwa vibanda hivyo ambavyo vimejengwa na kuendelea kujengwa kila kukicha na kusababisha kupungua eneo la kituo hicho kinachokadiriwa kuhudumia magari kati ya 50 na 70. Madereva  hao walidai kuwa wamekuwa wakilipa ushuru lakini hawatendewi haki ikiwa ni pamoja na kufanyiwa maboresho ya miundombinu.

Kutokana na ujenzi wa vibanda hivyo, kuna hatari ya kutokea majanga ya moto hasa baada ya kushamiri kwa vibanda vya mama lishe wanaopika kituoni hapo. Hali hiyo pia ni hatari kwa usalama wa magari, watu na mali zao na inaonesha kuwa wahusika hawaoni hayo yote kwa kuwa kuna viashiria vya kuwapo kwa vitendo vya rushwa.

Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, Elias Kayandabila, alipoulizwa kuhusu hayo, alisema amepokea taarifa japo yuko likizo licha ya kwamba alisema yeye ndiye chanzo cha yote na kwamba amekuwa akiibua moja baada ya lingine na atasimamia, kutekeleza maagizo yote na kuchukua hatua stahiki haraka.