Japan yaipatia Tanzania bil. 354/- za kuendeleza kilimo

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 11:29 AM Jan 15 2025
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba na Balozi wa Japan nchini anayemaliza muda wake, Yasushi Misawa, wakitiliana saini hati ya mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Ubalozi wa Japan, katika Ofisi Ndogo za Hazina, jijini Dar es Salaam jana.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba na Balozi wa Japan nchini anayemaliza muda wake, Yasushi Misawa, wakitiliana saini hati ya mkataba kati ya Serikali ya Tanzania na Ubalozi wa Japan, katika Ofisi Ndogo za Hazina, jijini Dar es Salaam jana.

SERIKALI ya Japan imepatia Tanzania mkopo nafuu wa Sh. bilioni 354.45 kwa ajili ya utekelezaji mradi wa uendelezaji kilimo vijijini.

Akizungumza mkoani Dar es Salaam jana baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba alisema mradi huo utatekelezwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ukisimamiwa na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Japan (JICA).

Alisema utekelezaji mradi huu utachochea ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kuongeza uzalishaji kwa wakulima kupitia upatikanaji wa mitaji nafuu.

"Hii itafikiwa kwa kutoa mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa wakulima, vikundi vya uzalishaji na taasisi zinazojihusisha na kilimo kwa kuziwezesha kuwekeza katika kilimo cha kisasa, kupata pembejeo bora na teknolojia ya juu ya kilimo," alisema Dk. Mwigulu.

Alisema msaada huo utachochea upatikanaji mitaji ya kilimo, wakulima kuwa na mazao mchanganyiko na kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi, ambako kutachangia usalama wa chakula, maendeleo vijijini na uimara wa uchumi kwa ujumla.

Alisema Tanzania imenufaika na ufadhili wa Japan kwa miaka zaidi ya 60 hasa kwenye sekta za kilimo, maji, afya, nishati, usafirishaji na elimu kupitia kujengewa uwezo.

Pia alisema Tanzania imeendelea kunufaika na ufadhili unaotolewa kupitia mashirika makubwa ya kimataifa ambako Serikali ya Japan inachangia kwa ajili ya miradi mingine ya kijamii na kiuchumi.  

Alisema msaada huo unaendana na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano ambao una maudhui ya kufikia ushindani na uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya watu ili kuongeza tija na uzalishaji kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Vilevile, alisema msaada huo unaendana na Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ambao unalenga kuimarisha na kuchochea matumizi ya zana za kisasa za kilimo, usalama wa chakula na lishe, kuwezesha upatikanaji wa masoko na kuwezesha uongezaji wa thamani.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan, Fujii Hisayuki alisema ushirikiano wa Japan na Tanzania ni wa muda mrefu na umejielekeza katika sekta muhimu.

Alisema sekta ya kilimo Tanzania imekuwa muhimu kwa uchumi kwa sababu imebeba asilimia kubwa ya wananchi ambao wengi wao wamejiajiri.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Mandeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), Frank Nyabundege, alisema tangu Rais Samia Suluhu Hassan aingie madarakani amekuwa ikiipa kipaumbele sekta ya kilimo ikiwamo kuongeza bajeti.

Alisema kwa miaka aliyokuwa madarakani (Rais Samia) ameipatia TADB zaidi ya Sh. bilioni 954 kwa ajili ya kuwawezesha wakulima kupitia mikopo nafuu.