IDADI ya wagonjwa wa kipindupindu imeongezeka jijini hapa na kufikia zaidi ya 340 kutokana na ulaji wa vyakula visivyokuwa salama kwenye mikusanyiko ya misiba.
Ofisa Afya wa Jiji la Mbeya, Odas Aron alisema juzi pekee walipokea wagonjwa 16 kutoka maeneo ambayo awali takwimu za mlipuko huo zilikuwa zimeanza kushuka.
Aron, alisema baada ya kufuatilia historia ya wagonjwa hao, walibaini wamekula vyakula kwenye misiba, licha ya serikali kupiga marufuku mikusanyiko ya aina hiyo na ulaji wa vyakula kwenye maeneo hayo.
Alisema vyakula vingi vinavyoandaliwa kwenye misiba vinakuwa si salama kutokana na uchafu na maji yanayotumika usafi wake wa mashaka.
“Tumejaribu kupiga marufuku mikusanyiko na ulaji wa vyakula kwenye misiba lakini watu wamekuwa wabishi kwa sababu ni utamaduni wao,” alisema.
Aliwataka wakazi wa jiji hilo kubadilika kwa kuacha kula ovyo, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni mara kwa mara kwa kuwa hali ya ugonjwa ni mbaya katika maeneo yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED