Polisi yawasaka walioiba vitu kwenye gari

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:22 PM Jan 14 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo.

Jeshi la Polisi mkoani Arusha linafanya uchunguzi pamoja na kuwatafuta watu wote waliohusika katika tukio la wizi ndani ya gari aina ya Toyota Alphard lenye namba za usajili T. 340 EJR kama inavyoonekana katika picha mjongeo kwenye mitandao ya kijamii.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Januari 14, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amebainisha kuwa tukio hilo lilitokea Januari 12 mwaka huu maeneo ya Kaloleni Jijini Arusha ambapo mtu aitwaye Goodluck Matingisa (41) anadai kuibiwa mali zake.

Kamanda Masejo amesema bado wanaendelea na uchunguzi kuhusina na tukio hilo na taarifa zaidi zitatolewa.

Aidha ametoa wito kwa wananchi kuacha tabia ya kubeba vitu vya thamani ndani ya magari yao bila kuwa na ulinzi na kuyaacha maeneo ya maegesho bila ya uangalizi wowote.

Sambamba na hilo amewaomba wananchi kuendelea kutoa taarifa za wahalifu na uhalifu ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wote watakaobainika.