KUANZIA Jumamosi wiki hii CCM, inakusudia kufanya Mkutano Mkuu Maalum ambao matokeo yake ni pamoja na kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti Bara.
Nafasi hiyo iliachwa wazi na Abdulrahman Kinana mwaka jana, aliyetangaza kujiuzulu na sasa chama kinaziba pengo hilo.
Wakati maandilizi yakiendelea, kuna baadhi ya majina yanayotajwa kwamba huenda miongoni mwao wakamrithi mwanasiasa huyo.
Licha ya majina yanayotajwa huku na kule, wapo baadhi ya wadau wa siasa wanaosema kuwa ni nyakati za usawa wa kijinsia na sasa nafasi hiyo ishikiliwe na mwanamama ili naye aonyeshe uwezo wake wa kukiongoza chama.
Baadhi ya wadau wa siasa na watetezi wa haki za wanawake na uongozi wanaotoa mchango wao ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Anna Henga.
Anasema tangu uhuru, chama hicho hakijawahi kuwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa mwanamke, na kwamba ni vyema sasa akapatikana.
Dk. Anna anasema hata kama mwenyekiti na makamu wake wakiwa wanawake si vibaya, kwa maelezo kwamba miaka yote katika nafasi hiyo wamekuwa ni wanaume na sasa ni vyema kinamama kushika nafasi hiyo.
Anasema suala la uongozi wa 50/50 lianze na lionekane kwenye ngazi za juu ili umma uione dhamira ya Tanzania kuwa na usawa wa kijinsia kwenye uongozi.
Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji huyo anatoa angalizo kuwa asiwe ilimradi mwanamke bali awe ambaye ana uwezo wa kuongoza, na kwamba hilo ndilo jambo la msingi linalopaswa kuzingatiwa.
"Sio kila mwanamke anafaa kuwa kiongozi bali kinachotakiwa kuzingatiwa uwezo wake wa kuongoza na ninaamini kuwa ndani ya chama hicho wapo wanawake wa aina hiyo," anasema Dk. Anna.
Anatamani kuona angalau nafasi hiyo inakuwa chini ya mwanamke ili kuendeleza kile ambacho chama kilianzisha tangu kuwa na makamu wa rais mwanamke na sasa ni Rais Mama Samia Suluhu Hassan.
Hatua hiyo ndiyo imefikia kuwa na mwenyekiti wa chama taifa mwanamke sasa, na kwamba mwendelezo huo ungefikia kuwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara mwanamama.
SAA YA WANAWAKE
Mkurugenzi wa Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni Dar es Salaam, Seleman Bishagazi, anasema sasa ni wakati sahihi kwa chama hicho kumpata makamu mwenyekiti mwanamke.
Anaongoza kuwa wanawake wengi wameelimika kuhusu masuala ya uongozi wa kisiasa, kiuchumi, kiteknolojia na hilo linawezekana.
"Vuguvugu la harakati za kutafuta usawa wa kijinsia katika uongozi, limesaidia kuwafanya wanawake kuwa na uelewa wa kutosha wa masuala ya uongozi, hivyo kwa mtazamo wangu ninaona ni zamu ya wanawake kuongoza CCM kwa sababu wapo," anasema Bishagazi.
Mbali na hilo, anasema wapo wasomi wanawake wengi katika chama hicho ambao wanaweza kukabidhiwa majukumu wakayatekeleza kwa ufanisi kama ambavyo wanaume wanafanya au pengine hata kuwazidi.
"Uongozi si mzigo wa kubeba begani au kichwani bali uwezo wa kuongoza, elimu na busara ninazoamini kuwa wanawake wengi wanazo lakini bado wameachwa nyuma hasa katika vyama vya siasa," anasema.
Bishangazi anafafanua kuwa kwa kuwa tangu kuanzishwa kwa TANU hadi CCM hajawahi kuwapo makamu mwenyekiti wa chama mwanamke, Mkutano Mkuu Maalum wa chama hicho kwa mara ya kwanza uweke mwanamke asaidiane na Rais Samia, kukiongoza chama.
"Mimi ni mwanaharakati ninazunguka maeneo mbalimbali ninaona jinsi wanawake walivyo na mwamko katika uongozi. Nina imani nao kuwa wanaweza kuongoza," anasema.
SI LAZIMA
Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Dk. Ananilea Nkya, anasema uongozi hauna jinsi bali kinachotakiwa ni kuwa na uwezo na sifa.
"Kwenye suala la uongozi, siangalii mwanamke au mwanaume kwa maumbile yake bali ninaangalia kama ana sifa ya uongozi. Hivyo, hata CCM wanapaswa kuzingatia hilo," anasema Ananilea.
Anasema kusukumwa na mtazamo wa mwanamke au mwanaume bila kuzichunguza sifa za mtu katika uongozi, kunaweza kusababisha ombwe na hata kuliangamiza taifa kwa kuongozwa na watu wasio na sifa na wala vigezo.
Kama nilivyoanza kueleza, kwangu mwanamke au mwanaume kwa maumbile, si kigezo cha kuwa kiongozi, bali uwezo na sifa za kuongoza ndivyo vinavyopswa kuzingatiwa," anasema.
Mwenyekiti huyo anataja baadhi ya sifa za kiongozi kwamba ni kuwa na karama na uwezo wa kuongoza, mkweli, anayejitambua, msimamizi wa maamuzi, msikilizaji na awe na umoja na wale anaowaongoza.
"Kwa ujumla sifa zipo nyingi kwa wanawake na wanaume, lakini tusing'ang'anie mwanamke au mwanaume kwa maumbile bali sifa za kuongoza ndizo ziwekwe mbele ili kupata kiongozi bora," anasema.
Anasema pamoja na sifa hizo, kiongozi anatakiwa kuwa na elimu itakayomwezesha kufanya kazi kwa ufanisi, na kwamba hata ndani ya CCM wapo watu wa aina hiyo, huku akifafanua kuwa upatikanaji wa makamu mwenyekiti CCM taifa usisukumwe na jinsia.
"Awe mwanamke au mwanaume wote wanafaa kuongoza ili mradi sifa za uongozi zizingatiwe bila kuegemea katika masuala ya jinsia ambayo yanaweza kusababisha asipatikane kiongozi bora ikiwa bora kiongozi anasema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED