Mbowe: Kuangamiza CHADEMA ni uhaini

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:14 AM Jan 14 2025
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Vijana wa  chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Vijana wa chama hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.

HUKU kukiwa na kauli tofauti juu ya hatima ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) dhidi ya mchakato unaoendelea wa uchaguzi wa viongozi wakuu, Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe amesema kuangamiza chama hicho hakuna tofauti na uhaini kwa kuwa kimebeba maono ya watanzania wengi.

Amesema kuwa kila mwanachama wa chama hicho anapaswa kumkataa shetani anayetaka kukifarakanisha chama hicho.

Mbowe alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Baraza la Wazee wa Chama hicho (BAZECHA) ambao ulitumika kuchagua viongozi wapya wa baraza hilo.

Mbowe alisema chama hicho ni bora na kikubwa kuliko mtu yeyote, awe kiongozi wa kitaifa, kwenye mabaraza yake au mwanachama.

Alisema yapo mambo mengi ambayo wamejifunza katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi huo, akiweka wazi kuwa tabia iliyojionyesha katika uchaguzi wa awamu hii si tabia za wana-CHADEMA waliojenga chama hicho kwa jasho na damu kwa zaidi ya miaka 30.

"Yako mengi ya kujifunza, tumeona minyukano ikitokea kwenye mitandao, miongoni mwa wanachana na viongozi, lakini ninachotaka kuwahusia wanachama wetu ni kwamba chama hiki ni bora na ni kikubwa kuliko yeyote miongoni mwetu. Kwa hiyo kila kiongozi bila kujali nafasi yake ndani ya chama au ndani ya mabaraza ana wajibu wa kukilinda," alisema.

Mbowe alisema anaamini chama hicho kitakuwa bora na kuimarika zaidi kama kitalindwa kwa umoja wao.

Alisema kuna baadhi ya watu ambao siyo wanachama wa chama hicho ambao wanashabikia kile kinachoendelea ndani na kuwataka wanachama wa chama hicho kukataa kuingia katika mtego wao.

"Tumkatae shetani na mbinu zake zote, wako wengine ambao siyo wana-CHADEMA, wana kiherehere na mambo ya CHADEMA, kuliko tulivyo wanachama, tukatae tuseme umoja wetu ni wa muhimu kuliko sifa ya mtu yeyote miongoni mwetu mmoja mmoja," alisisitiza Mbowe.

ALIVYOKABIDHIWA CHAMA

Mbowe alitumia jukwaa hilo kuwasimulia wajumbe hao namna alivyokabidhiwa chama hicho kukiongoza kwa mara ya kwanza mwaka 2004 katika nafasi anayoishikilia hadi sasa, huku akigusia alivyofanya mabadiliko.

"Nilipokabidhiwa chama hiki mwaka 2004, kilikuwa hakina mabaraza, kulikuwa kuna kamati ya taifa ya vijana na kamati ya taifa ya kinamama. Wakati wazee wananikabidhi, niliwaambia kwamba kama mnataka niwe kiongozi wa chama hiki, nitafanya mabadiliko makubwa ya Katiba ya chama, tuingize mawazo, mikakati ya kukipanua chama hiki.


"Wakati ninakabidhiwa hata bendera yetu ilikuwa ya rangi moja, kwa hiyo tukakubaliana kwamba tunabadilisha Katiba, tukaanzisha mabaraza ya chama, kulikuwa hakuna kanuni ya uendeshaji, hakukuwa na itifaki lakini haya yote tuliyapata si kwa ajili ya Mbowe, ni kwa sababu tulifanya kazi katika umoja wetu, tukiweka mawazo yetu pamoja," alisema.

Mbowe alisema hata sasa bado ipo nafasi ya kila mwanachama wa chama hicho kutoa mawazo yake ya namna anavyoona chama hicho kinaweza kufanyiwa maboresho kulingana na Katiba inayokiongoza.

"Hata leo tuna wajibu wa kuweka mawazo yetu pamoja, yeyote miongoni mwetu anayefikiria kuna mambo yakifanyika, yatakifanya chama hiki kiwe bora zaidi, milango iko wazi, hatuna sababu ya kulumbana. Kama kuna mambo ya kurekebisha tufanye kwa namna ambavyo Katiba yetu imeruhusu kwa umoja, upendo, kwa kushirikishana.

"Haya yote yanawezekana kwa sababu chama cha siasa, Katiba, kanuni, maadili na miongozo yake ni nyaraka zinazoishi wala si kama vitabu vitukufu vya Mungu ambavyo vikiandikwa haviwezi kubadilishwa kila siku," alisema Mbowe.

Alisema kama dunia inaishi na mabadiliko, hata chama kinaweza kufanya maboresho, hivyo CHADEMA nacho kinaweza kufanya hivyo.

"Dunia inaishi, yanatokea mabadiliko ya kiteknolojia, ya kijamii na kiuchumi ambayo yanapelekea ulazima wa kufanya rejea na kurekebisha mambo kadri muda unavyokwenda na mahitaji ya wakati. "Kwa hiyo tusitafute sababu yoyote ya kuleta ugomvi miongoni mwetu, kila mmoja ailinde taasisi hii, tunapoona kuna cha kurekebisha, tushauriane, turekebishane kujenga umoja na mshikamano wetu," alisema Mbowe.

Mwenyekiti huyo pia alionya tabia ya vijana wa chama hicho kuwabeza wazee waliotumikia chama hicho.

"Juzi nilikuwa ninaongea na vyombo vya habari, nikakemea tabia moja ambayo inaanza kujengwa na vijana kufikiri uzee ni laana na kutokuuona kama busara, kutokuuona kama uzoefu na kutokuona uzee kama maktaba ya chama, kwamba tunaweza kuwa na ujasiri wa kuwahukumu viongozi ambao wana umri mkubwa katika chama chetu."Kwamba tukishafikia umri wa kustaafu, ninyi wazee hamna thamani ndani ya chama hiki, haiwezekani! Ngoma ya watoto haikeshi, ninataka wakati wetu tuwatambue wazee,” alisema Mbowe.

NIDHAMU

Mbowe pia alisema chama hicho hakiwezi kujengwa kuwa imara kwa matusi na kukashifiana bali kitafanikiwa endapo kutakuwa na nidhamu.

“Hatuwezi kujenga chama cha ukombozi wa nchi kama kila mmoja hawezi kumwona mwenzake kama bega la kulilia katika mapambano, si kweli kwamba kutwezana, kutukanana, kukashifiana, kudhalilishana, kunaweza kuwa sehemu ya kukijenga chama imara. Leo nilikuwa namwuliza (Tundu) Lissu kwamba hawa vijana wa moto kwelikweli, hivi walizaliwa mwaka gani?

“Kwa waliokuwapo miaka 30 ya ujenzi wa chama walishirikiana, walijengana, lakini kwa tabia iliyooneshwa kwenye uchaguzi wa awamu hii, si utamaduni wa CHADEMA.

“Mtambue kwamba kila mmoja wenu anamwitaji mwingine, tunahitajiana wote kama familia ili kutimiza malengo yetu, pepo lolote lenye dhana ya kututenganisha hatupaswi kulilea, lishindwe kwa nguvu zote,” alisema Mbowe.

Mwenyekiti huyo alisema ni sahihi kutofautiana pindi uchaguzi unapokaribia, lakini ni vyema pia watu wakaimarisha umoja wao.

Mbowe alisema: “Ni kweli tutanyukana, tukaonana kwenye boksi lakini tukimaliza lazima tushikane mikono kutafuta fomula kwamba tunahitajiana, tunataka chama hiki watoto wa watoto wenu wakakikute kikiwa imara kuliko jana na si kwa kutukanana.

“Tuinue taasisi hii ambayo iliundwa kwa jasho, damu na machozi ya watu. Hatupaswi kuendekeza hili, hivi vyeo vinapita, malengo yetu ni ya msingi kuliko nafasi ya kila mmoja wetu, tunawahitaji wazee, tunawahitaji vijana jeuri, tunawahitaji wazee imara, tunahitaji kinamama, tunahitajiana, tupendane tuvumiliane, tuijenge familia ya CHADEMA.”

TUNDU LISSU

Naye Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Lissu, alisema vijana ndiyo nguvu ya mabadiliko na kuwataka wachague viongozi ambao watakuwa jasiri watakaoongoza mapambano pasipo kukimbia pindi mambo yanapokuwa magumu.

Akizungumza katika mkutano wa BAZECHA, Lissu aliwataka wajumbe hao kuwachagua viongozi ambao watawaongoza vyema na kwa haki katika miaka mitano ijayo.

“Niwatakie kila la heri katika uchaguzi huu, tuchague viongozi watakaotuongoza vyema katika miaka mitano inayokuja, tuchague viongozi kwa uchaguzi ulio huru, wa haki na wa wazi kama yanavyosema maneno ya Katiba yetu,” alisema Lissu.

Mwanazuoni Dk. Azaveli Rwaitama aliwaonya wapambe wanaoshabikia wagombea katika uchaguzi huo, akisema watu hao ni hatari kuliko wagombea wenyewe.

Pia alitoa hadhari kwa atakayechaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho kuepuka kiburi.

Uchaguzi wa viongozi wa ngazi za juu wa chama hicho unatarajiwa kufanyika Januari 21 mwaka huu, huku macho na masikio ya wengi yakielekezwa kwa atakayeshinda nafasi ya uenyekiti, Mbowe na Lissu wakiwa miongoni mwa wanaoiwania.