Mgogoro wa ardhi ulivyoua, kujeruhi ndugu

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 04:32 PM Jan 14 2025
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Benjamin Kuzaga.
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Benjamin Kuzaga.

JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za mauaji ya watu wawili na kujeruhi wengine watano baada ya kuzuka mgogoro wa ardhi katika Kijiji cha Luhanga Wilaya ya Mbarali.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Benjamin Kuzaga alisema tukio hilo lilitokea Januari 10, mwaka huu baada ya kutokea ugomvi baina ya familia ya Mzee Rafael Mjengwa mwenye hati namba MBL/420 iliyotolewa mwaka 1987 dhidi ya familia ya Mzee Malewa.

Alisema ugomvi huo umesababishwa na mgogoro wa shamba lenye ukubwa wa ekari 1050 baada ya familia ya Malewa kudai  ni mali yao kwa ajili ya kilimo na kulisha mifugo kwa muda mrefu.

Alisema familia ya Mzee Rafael Mjengwa wakiwa wanaendelea na maandalizi ya kilimo katika shamba hilo, ghafla walishambuliwa na kundi la watu wapatao 15

wanaodaiwa kuwa ni wa Mzee Malewa na kusababisha mauaji hayo na majeruhi hao. 

Aliwataja watu hao waliouawa kuwa ni Iddi Mjengwa (38), Mkazi wa Igurusi na Maige Jifaru (44) wa Isunura wilayani humo. 

 Kuzaga alisema baada ya polisi kupata taarifa za mauaji hao walifanya msako Januari 13 usiku  na kuwakamata watuhumiwa hao, Kuva Zengo (25), Lukeresha Mlawa (32) na Bulanda Mathias (25), wakazi wa Kijiji cha Luhanga.

 Awali akielezea  tukio hilo, msemaji wa familia ya Rafael Mjengwa iliyofiwa na ndugu yao, George Zima alisema wakiwa kwenye shamba lao ulifika msafara wa pikipiki tisa, magari mawili na watu waliokuwa wamebeba  majembe na kuwavamia.

Aliomba serikali kupitia Wizara ya Ardhi kushughulikia mgogoro huo ambao umedumu kwa muda mrefu kwa madai kuwa kabla ya kutokea tukio hilo la mauaji, walivamiwa zaidi ya mara tatu na familia ya Malewa.

“Tunaomba serikali itusaidie kwa sababu tatizo hili limekuwa kubwa na linatusababishia matatizo, tulishawahi kuwasilisha Kamati ya Siasa ya CCM na walitoa maagizo,” alisema Mjengwa.

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Maulid Surumbu aliwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake wanapokuwa na migogoro wafuate taratibu kutatua.