JKT Queens yatamba ipo vizuri kuchapa wote GIFT

By Shufaa Lyimo , Nipashe
Published at 08:22 AM Jan 15 2025
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Esther Chabruma.
Picha: Mtandao
Kocha Mkuu wa timu hiyo, Esther Chabruma.

BENCHI la Ufundi la Timu ya JKT Queens wenye umri chini ya miaka 17, limesema halina wasiwasi kukutana na timu yoyote katika mashindano ya CAF U-17 Girls Integrated Football Tournament (GIFT), yanayoendelea katika Uwanja wa Azam Complex, Chamanzi, Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Jumatatu usiku  baada ya kumalizika kwa mchezo wao dhidi ya City Lights FC ya Sudan Kusini na kushinda mabao 10-0, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Esther Chabruma, alisema amefurahishwa na ushindi walioupata licha ya kutokuwa rahisi. 

"Nipo tayari kukutana na timu yoyote kwa kuwa nina matumaini makubwa na timu yangu, ninawashukuru pia mashabiki kutokana na ushirikiano wanaotuonesha tunapokuwa uwanjani," alisema Chabruma. 

Akizungumzia mchezo huo, alisema waliingia wakiwa na tahadhari kuhakikisha wanapata pointi tatu jambo ambalo limewafanya wapate idadi kubwa ya magoli.

Kocha huyo alisema siri ya mafanikio yao imetokana na wachezaji wake kufuata maelezo anayowapa, nidhamu pamoja na ushirikiano waliokuwa nao.

Alisema anashukuru hana majeruhi yeyote kwani wachezaji wake wote wanaendelea vema kiafya.

Kwa ushindi huo wa mabao 10-0 dhidi ya City Lights FC, JKT Queens imefikisha pointi 9 huku ikiendelea kuongoza katika Kundi A.

Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa City Lights, alidai kuwa wameshindwa kufanya vizuri kutokana na wachezaji wake kuwa na umri halali tofauti na ukiwalinganisha na wapinzani wao. 

"Tumeshindwa kufanya vizuri kwa kuwa tumekutana na wachezaji wenye umri zaidi ya miaka 17,  hivyo waliwazidi nguvu wachezaji wangu," alisema