NI simulizi iliyojaa simanzi na vilio. Wananchi walijitokeza kutoa msaada wa haraka wa kuwaokoa majeruhi wa ajali, wanapoteza maisha kwa kuparamiwa na lori lenye shehena ya saruji lililopoteza mwelekeo.
Ni mkasa uliogharimu maisha ya watu 11 huku wengine 12 wakiwa majeruhi baada ya kukanyagwa na lori aina ya VOLVO lenye namba za usajili T 782 BTU lililokuwa linatokea Tanga kwenda Arusha.
Imeelezwa kuwa lori hilo lilipata hitilafu katika mfumo wa breki kisha kupoteza mwelekeo na kuwagonga watu hao eneo la Chang’ombe, Kata ya Segera, Wilaya ya Handeni.
Akieleza jana chanzo cha ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Almachius Mchunguzi alisema ajali hiyo ya VOLVO ilitokea saa 3:30 usiku wa Januari 13 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu hao.
Kwa mujibu wa ACP Muchunguzi, ajali hiyo ilitokea baada ya VOLVO kuwagonga watu waliokuwa wanashangaa ajali nyingine ya basi la abiria, namba T 720 EJP aina ya TATA, lililokuwa limeteleza na kuacha barabara bila kusababisha madhara yoyote kwa binadamu.
"Jeshi la Polisi linamsaka dereva aliyejulikana kwa jina la Baraka Meleckdezeck, maarufu Urio, aliyekuwa anaendesha VOLVO kutokana na kugonga watu waliokuwa pembeni mwa barabara wakiangalia ajali iliyokuwa imetokea katika eneo la Chang’ombe.
"Gari namba T 720 EJP aina ya TATA basi, lilikuwa limeteleza na kuacha barabara bila kusababisha madhara yoyote kwa binadamu," alisema.
Waliofariki dunia na kutambuliwa katika ajali hiyo ni Hamisi Mkumbuka (Saa Mbovu), Bujaga Rashid, Adamu Maneno (Mkweguto), wote wakazi wa Maili Kumi, wilayani Handeni.
Wengine ni Sawebu Juma (Kashaija), mkazi wa Dar es Salaam, Joseph Mboye, Nasib Shemsanga, Twalib Kashaija, Ignatus Shayo, Rashid Yahaya, Salim Abdurahaman na mwingine ambaye mwili wake haujatambuliwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Muchunguzi, majeruhi 12 wamepelekwa Hospitali ya Magunga, wilayani Korogwe kwa ajili ya matibabu.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Dk. Paul Patrick, alisema wamepokea majeruhi wa ajali hiyo; wanne wamehamishiwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga (Bombo) na watatu wamefariki wakiwa wanapatiwa matibabu.
Alisema hospitalini huko kuwa wamebakiwa na majeruhi saba ambao wanaendelea na matibabu.
MAJERUHI ALONGA
Mmoja wa majeruhi wa ajali hiyo, Faraji Karata alisema kuwa aliposikia ajali hiyo, alikimbia kwenda kutoa msaada kwa majeruhi na kuimarisha ulinzi, lakini alijikuta akipatwa na ajali.
"Wakati lori hilo la VOLVO linakuja tuliliona, lakini hatukuelewa ilikuwaje likatufikia na kuua wenzetu na sisi kujeruhiwa. Ninashukuru Mungu kwa kuniokoa, sasa hivi ninaendelea na matibabu," alisema Karata.
SERIKALI YABEBA MSIBA
Mkuu wa Mkoa huo, Balozi Dk. Batilda Buriani, alisema jana kuwa serikali itabeba gharama za maziko ya watu hao pamoja na matibabu ya majeruhi 12.
"Serikali itagharamia matibabu kwa wale wote walioathirika na ajali hii na itagharamia usafiri kwa waliofariki dunia. Tunatoa ubani kwa wale wote waliofiwa na jamaa zao na kuwapa sanda na kuwasitiri," alisema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED