CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema hakihusiki kwa namna yoyote au jambo lolote na uchaguzi mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kuwa kina mambo mengi ya msingi ya kufanya.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makala, alisema hayo jana wakati akizungumza na moja ya vyombo vya habari kuhusu maandalizi ya Mkutano Mkuu wa CCM, utakaofanyika mwishoni mwa wiki hii.
Makala alisema hayo wakati akijibu swali la mwandishi aliyehoji kuwa CCM inazungumziaje maneno ambayo yamekuwa yakisemwa na baadhi ya watu kuwa inahusika na kuchochea mvutano uliopo hivi sasa ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani.
“Nitumie nafasi hii kama msemaji wa chama kwamba CCM haikusiki na jambo lolote na uchaguzi wa CHADEMA. CCM tunayo majukumu mengi ya kufanya na viongozi wote na watendaji mawazo yetu yote, akili zetu na nguvu zetu zote tumezielekeza kwenye mkutano mkuu huu maalum. Hatuwezi kuhangaikia kujihusisha na kazi za chama kingine. Kwanza tunajihusisha kwa tija ipi na kwa faida ipi?
“Kwa hiyo mimi niseme tu kwamba hayo ni maneno ambayo wanasema wao wenyewe kambi zao hizo zinachafuana. Kwa hiyo ndiyo mambo ambayo nimejifunza kwamba kuna hela chafu kuna mnyukano ni jambo ambalo najifunza ndani ya chama hicho ambako uchaguzi unaendele. Kwa hiyo CCM isihusishwe na jambo lolote. Tuna mambo mengi ya msingi ya kufanya,” alisisitiza.
Makala pia alisema anakitakia uchaguzi mwema chama hicho, kipite salama katika mnyukano huo mkali na kuwapata viongozi wengine watakaokiongoza.
“Tunawatakia kila la heri kwa maana tunayasikia mengi na sisi tunawaombea wavuke salama kwani CCM inahitaji upinzani wenye nguvu na tunatumaini kuwa watatoka salama kwenye mnyukano huu na kuwapata viongozi wao,” alisema.
Pia alisema mikutano hiyo miwili (CCM na CHADEMA) ina utofauti mkubwa kuilinganisha kwa kuwa wa CCM ni wa watu wenye furaha huku CHADEMA wakiwa wa mtifuano.
“CCM kwa kweli tumejipanga ni mkutano wa aina yake. Tuna viongozi, mabalozi, wageni wajumbe 1,950 na waalikwa zaidi ya 3,500. Hivyo kwa kigezo cha kujifunza ni kwamba CCM haina la kujifunza kwa CHADEMA kwa kuwa mkutano wetu ni wa aina yake,” alisema.
Makala alisema maandalizi ya mkutano mkuu maalum wa kihistoria wa chama wenye ajenda kuu tatu, yamekamilika.
Alisema mkutano huo utakuwa na kazi ya kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa Chama, kupokea taarifa za utekelezaji Ilani kwa serikali mbili ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, na kupokea taarifa ya kazi za chama katika kipindi cha 2022/2025.
“Maandalizi kwa kiasi kikubwa yamekamilika, Dodoma kumekucha tunawakaribisha wajumbe wote wa mkutano mkuu na waalikwa kuja,” alisema.
Kuhusu mchakato wa kumpata Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, alisema hiyo ni nafasi ya juu na kwamba ni msaidizi wa juu wa mwenyekiti wa chama, hivyo wanakuwapo wawili Bara na Zanzibar.
“Kama unavyofahamu nafasi hii ilikuwa wazi baada ya (Abdulrahman) Kinana kuomba kupumzika. Umefika wakati mwafaka wa kujaza nafasi hiyo, hivyo utaratibu ni kwamba nafasi hii haigombewi, hujazi fomu, haina kinyang’anyiro. Inaanzia mchakato wake katika Kamati Kuu kufikiria na kutoa mapendekezo ya mtu anayefaa kujaza nafasi hiyo,” alisema.
Baada ya hapo, alisema jina litapelekwa NEC ambayo ikiridhia na kupitisha, jina hilo litapelekwa kwenye Mkutano Mkuu ili wajumbe wapige kura za ndiyo na Hapana. Huo ndio mchakato wa kumpata Makamu Mwenyekiti,” alibainisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED