Majeruhi wanane ajali ya VOLVO wahamishiwa Bombo

By Oscar Assenga , Nipashe
Published at 02:08 PM Jan 15 2025
Majeruhi wanane ajali ya VOLVO wahamishiwa Bombo.
Picha:Mtandao
Majeruhi wanane ajali ya VOLVO wahamishiwa Bombo.

HALI za majeruhi 13 wa ajali ya barabarani katika eneo la Chang’ombe, Maili Kumi, Wilaya ya Handeni, walioparamiwa na lori lililokuwa limebeba shehena ya saruji zinaendelea kuimarika taratibu, huku wanane kati yao wakihamishiwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga ya Bombo.

Ajali hiyo iliyotokea majira ya saa 3:30 usiku wa Januari 13 mwaka huu, ikihusisha lori aina ya VOLVO, lenye namba za usajili T 782 BTU likitokea Tanga kwenda Arusha, ilisababisha vifo vya watu 11.

Akizungumza leo (Januari 15, 2025) na Nipashe Digital, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe (DMO), Dk. Mariam Cheche, amesema uamuzi wa kuwapa rufani majeruhi hao, unalenga kutoa fursa ya kupata matibabu ya kibingwa kutokana na kuvunjika vibaya.

Kwa mujibu wa Dk. Cheche, waliobaki katika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe ya Magunga, ni wanaume wanne na mwanamke mmmoja, ambao hali zao zinaendelea kuimarika, baada ya kupata huduma za matibabu.

Hata hivyo, alipotafutwa Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Tanga ya Bombo, Dk. Frank Shega kuzungumzia hali za majeruhi waliohamishiwa hapo, amesema ni kweli wamepokea majeruhi wanane, ambao wapo wodini wakiendelea na matibabu.

Amesema majeruhi hao, baada ya kupokelewa walianza kupatiwa huduma mbalimbali ili kuwawezesha kuimarika kurudi katika hali zao za kawaida.