TAASISI ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI) imewaomba watanzania kujitokeza kuichangia damu ili kuokoa maisha ya majeruhi wanaohitaji huduma hiyo.
Ombi hilo lilitolewa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Uuguzi wa MOI, Cresencia Mwibari wakati akijibu hoja na maoni ya wagonjwa na ndugu wa wagonjwa eneo la kusubiria huduma lililoko katika taasisi hiyo.
Cresencia alisema kuwa uhitaji wa damu ni mkubwa. Kwa siku taasisi hiyo hutumia wastani wa chupa 20 hadi 30 kwa ajili ya majeruhi wa ajali mbalimbali zikiwamo za barabarani.
"Ninapenda kutoa rai kwa watanzania wenzangu kuja kuchangia damu katika taasisi ya MOI, hii ni hospitali ambayo inahudumia majeruhi wa ajali mbalimbali, wagonjwa wanakuja wakiwa wamepata majeraha wamemwaga damu, kwahiyo asilimia kubwa wagonjwa huongezwa damu.
"Taaasisi yetu (MOI) hutumia chupa 20 hadi 30 za damu kwa siku, tukipata watu watakaokuja kuchangia damu itasaidia na damu itapatikana kwa wingi na kutuwezesha kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, tunaomba watu waje kwa wingi," alisema.
Cresencia aliwakumbusha wachangiaji damu salama wa muda mrefu wanaofika katika taasisi hiyo kupatiwa huduma za matibabu kwenda na kadi zao za uchangiaji damu na kuziwasilisha katika idara ya maabara ya MOI kwa ajili ya kufanyia uhakiki na uthibitisho.
Mmoja wa waliowahi kuhudumiwa na taasisi hiyo, Philimon Ndaki aliwapongeza watumishi wa MOI kwa kumpatia huduma za kuridhisha za matibabu, akifafanua kuwa alifanyiwa upasuaji miaka minne iliyopita na sasa anaendelea vizuri na kuhudhuria kliniki kila baada ya miezi sita katika Taasisi hiyo.
"Nilikuja nikiwa na hali mbaya lakini matibabu ya kibingwa niliyopata hapa yaliniwezesha kupata nafuu kubwa sana na sasa niko vizuri sana, watumishi wa MOI ni wakarimu sana," alisema
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED