MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ,Tundu Lissu amesema chama hicho na wafuasi wake wapo tayari kupata maumivu wakidai mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi nchini.
Akizungumza na wakazi wa Manyoni mkoani Singida alipokwenda kufanya ziara ya kichama, Mwenyekiti huyo amesema chama hicho hakipo tayari kushiriki uchaguzi bila kwanza kufanyika mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi.
“Tunafahamu tukienda kwenye uchaguzi bila mabadiliko katika mfumo wa uchaguzi tunaenda kuumia na hatupati chochote” amesema Lissu
“Mnakumbuka ugomvi wetu mwaka jana kwenye kuapisha mawakala , tulifanyiwa kila aina ya uovu ili kuhakikisha kwamba hatuna mawakala na wale waliofanikiwa kuapishwa kuingia vituoni ilikuwa ni mbinde” amesema Lissu.
Lissu alidai idadi ya wenyeviti wa mitaa 87 waliyoipata katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi Novemba mwaka jana hakiendani na matarajio yao kwa kulinganisha na uchaguzi kama huo uliofanyika mwaka 2014 miaka 10 iliyopita ambapo alidai katika jimbo la Singida Mashariki pekee walipata mitaa 47 kati ya 50.
Lissu ametaka Tume ya Uchaguzi kupewa mamlaka ya kuajiri wafanyakazi wake yenyewe badala ya kutegemea watumishi wa umma ambao amedai wanaingiliwa kimaamuzi na wakuu wao wa kazi na hivyo kushindwa kuwa huru kufanya shughuli za uchaguzi.
“Novemba mwaka jana mitaa ile ya mjini kwa nchi nzima tumeshinda mitaa 36 tu katika mitaa zaidi ya 4000 iliyopo nchi nzima, miaka 10 iliyopita tulishinda mitaa zaidi ya 1500 nchi nzima sasa hilo linawezekanaje” alihoji Lissu.
Alisema watumishi wa umma kutokusimamia uchaguzi ili kuondoa uwezekano wa uchaguzi kuvurugwa kwa kile alichosema kutishwa na mabosi wao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED