Majaliwa awataka wana CCM kujipanga kwa uchaguzi

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 05:33 PM Feb 15 2025
Kassim Majaliwa
PICHA:MPIGAPICHA WETU
Kassim Majaliwa

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amewahimiza wananchi wa Itilima kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuunga mkono chama hicho kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza kwenye Mkutano mkuu wa CCM wilayani Itilima mkoani Simiyu, Majaliwa amewataka wanachama wa chama hicho kuendelea kueneza mafanikio yaliyopatikana kupitia serikali ya CCM ili wagombea wa chama hicho wasipate kazi kubwa katika kampeni.

"Mwaka huu ni wa uchaguzi mkuu, vyama vyote vitakuja kuomba kura, lakini nyinyi mnajua kuwa CCM inapeleka wagombea wake katika nafasi za Urais, Ubunge na Udiwani. Kwa nafasi ya Urais, mgombea wetu ni Rais Samia Suluhu Hassan, na kwa Zanzibar ni Hussein Mwinyi watazunguka nchi nzima kuomba ridhaa yenu," amesema Majaliwa.

Pia amewasisitiza wananchi wa eneo hilo kuelewa na kushiriki kusambaza taarifa za mafanikio yaliyopatikana katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu, afya, maji, umeme, kilimo na mifugo, ili kuwawezesha wagombea wa CCM kupita kwa urahisi katika uchaguzi huo.

"Leo mnaelewa kazi iliyofanywa na serikali yenu na mbunge wenu. Tunapaswa kuyaeleza haya kwa wengine ili wagombea wetu wasipate kazi ngumu. Wananchi wa Itilima wanapaswa kuwa na uelewa wa hali ya juu kuhusu maendeleo haya," amesema.

Katika sekta ya afya, Majaliwa ameeleza kuwa wilaya hiyo tayari ina zahanati 37, na lengo ni kuhakikisha kila kijiji kinakuwa na zahanati yake ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi.

"Tunataka mwananchi apate huduma za afya karibu na makazi yake. Hongera sana Mbunge Njalu Silanga kwa kuhakikisha wilaya hii inapata zahanati nyingi. CCM itaendelea kuhakikisha mbunge wenu anapata ushirikiano wa serikali ili huduma zote zipatikane hapa Itilima," amesisitiza.

Kuhusu barabara, Waziri Mkuu amekiri kuwa kuna changamoto ya barabara za vumbi, hasa wakati wa msimu wa mvua, akiahidi kuwa serikali itaendelea kuzifanyia maboresho kupitia Wakala wa Barabara (TARURA).

"Mbunge endelea kuwasilisha orodha ya barabara zilizoharibika ili fedha zipatikane na TARURA izitengeneze. Serikali inatambua umuhimu wa barabara katika maendeleo ya wananchi," amesema.

Mkutano huo umelenga kuwasilisha utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2020/25 jimboni Itilima, huku viongozi na wananchi wakionesha mshikamano mkubwa katika kuunga mkono chama hicho.