Zimesalia saa chache tu, ambapo bara la Afrika na hususan mgombea kutoka Kenya, Raila Odinga kujua hatima yake ikiwa atakuwa mrithi wa Moussa Faki Mahamat kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Uchaguzi unaandaliwa leo Februari 15, katika kikao cha Marais ambacho kinatarajiwa kukamilika Jumapili Februari 16.
Waziri huyo Mkuu wa zamani wa Kenya mwenye umri wa miaka 80 anaingia kwenye kinyang'anyiro kikali dhidi ya Mahmoud Ali Yousuf wa Djibouti na Richad Randrimandrato wa Madagascar.
Daktari Peter Mwencha, ambaye ni mhadhiri wa Diplomasia na Ofisa Mkuu wa chama cha wataalamu wa masuala ya kimataifa (IRSK) anasema kibarua kitakuwa kigumu kwa mwanasiasa huyo kutoka eneo la Afrika Mashariki.
"Kenya imefanya kampeni kali katika muda huu wote. Raila amejiwasilisha vyema kwa viongozi muhimu katika maeneo yote ya bara, japo kumekuwa na uungwaji mkono wa kampeni yake miongoni mwa Wakenya. Kilichosalia sasa ni kusubiri uchaguzi ufanyike," alisema Dk. Mwencha katika mahojiano na BBC.
Huku viongozi hao watatu wakijiandaa kwa kura hiyo ambayo imesubiriwa na wengi barani na hata nje ya bara, tangazo la Sekretarieti ya Jumuiya ya Maendeleo ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuyataka mataifa wanachama kumuunga mkono mgombea wao aliyekuwa Waziri wa mambo ya kigeni wa Madagascar Richard Randrimandrato, kumezua mjadala mkali miongoni mwa Wakenya ikiwa kura alizotarajia "Baba" kama anavyofahamika nchini Kenya, zitapungua na kumuondolea nafasi ya kumrithi Bwana Mahamat ambaye anaondoka mamlakani baada ya kuhudumu kwa miaka minane.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED