MTU Mmoja amefariki dunia na wengine kuwekwa chini ya uangalizi maalum katika Halmashauri ya Wilaya ya Musoma mkoani Mara, baada ya kukubwa na ugonjwa wa kuhara na kutapika.
Akitoa taarifa ya hali ya mlipuko wa ugonjwa huo, Mkuu wa Idara ya Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Musoma, Dk. Joseph Fwoma mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Maraa, Kanali Evans Mtambi, aliyetembelea kituo hicho kilichopo katika zahanati ya Kijiji cha Bwai.
Amesema mlipuko huo ulitokea Januari 23, mwaka huu.
"Januari 23 mwaka huu, halmashauri yetu ilipata wagonjwa 63, mmoja kati yao alifariki dunia na wengine kuruhusiwa baada ya kupona lakini tisa wanaendelea na matibabu katika kituo hiki," amesema Dk. Fwoma.
Aidha, amesema tatizo hilo linatokana na kuwapo kwa mwalo mkubwa wa wavuvi katika eneo na kwamba wamechagua Zahanati ya Kijiji cha Bwai, iliyokaribu na eneo hilo kuwa kituo cha kuwahudumia wagonjwa.
"Jitihada mbalimbali zimefanywa na halmashauri pamoja na mkoa ikiwa ni pamoja na kuwahamishia kwa muda wataalamu wengi wa afya katika kituo hiki, ili kuongeza nguvu za kuwahudumia wagonjwa," amesema.
Amefafanua kuwa wameweka dawa za kutosha, kusambaza dawa za kutibu maji, kuwahamishia wagonjwa wa kawaida katika majengo mapya ya Kituo cha Afya cha Bwai, kilichopo jirani na eneo hilo na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huo.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, amesema wilaya inaendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuwahamasisha wananchi kujenga na kutumia vyoo bora, hasa katika vijiji vilivyoko kando kando ya Ziwa Viktoria.
"Tayari jitihada mbalimbali zimeshafanyika ikiwamo kuwaagiza RUWASA wilaya ya Musoma kukamilisha kwa haraka mradi wa maji unaotekelezwa katika Kata ya Busambara, ili wananchi wa eneo hili wapate maji safi na salama," amesema Chikoka.
Aidha, ameahidi kuongeza nguvu kwa kufanya operesheni maalum ya kutoa elimu eneo hilo na kuhamasisha ujenzi na matumizi ya vyoo, kuchemsha maji ya kunywa na kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.
Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Bwai, Dk. Justus Haule, amesema hadi wakati mkuu wa mkoa anatembelea kituo hicho, kilikuwa na wagonjwa tisa, huku wagonjwa saba kati yao wakiwa ni wanaume.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Mtambi, amewaagiza wakuu wa wilaya pamoja na wataalamu wa afya halmashauri kuanzisha operesheni maalum ya kukagua usafi wa vyoo katika maeneo mbalimbali, ikiwamo kambi za wavuvi na masoko.
"Wakuu wa wilaya na wataalam wa afya wa halmashauri tokeni ofisini muanzishwe operesheni maalum ya kukagua vyoo bora na salama na matumizi ya vyoo hivyo na hasa maeneo yenye mikusanyiko kama kambi za wavuvi, masoko na majengo ya huduma mbalimbali kuhakikisha yana vyoo vinavyotumiwa na wananchi," amesema Kanali Mtambi.
Aidha, amewataka kufanya kampeni maalum ya ujenzi wa vyoo katika maeneo yaliyokumbwa na tatizo hilo na kushughulikia vyanzo vyote zinavyoweza kusababisha kuendelea kwa hali hiyo katika maeneo yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED