Katika hatua mpya ya mzozo unaoendelea Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kundi la waasi wa M23 likishirikiana na Muungano wa Mto Kongo (AFC) limetangaza kuwa wanajeshi wa zamani wa Jeshi la FARDC waliokamatwa au kujisalimisha wamehitimu mafunzo ya kiitikadi na mbinu za kijeshi.
Katika chapisho la M23 kwenye mtandao wao wa X leo Februari 18, picha zilionyesha wanajeshi hao wakiwa na sare na silaha rasmi za wanamgambo hao. Ujumbe uliambatana na chapisho hilo ulieleza:
"Wanajeshi wa zamani wa FARDC, waliokamatwa au kujisalimisha, wamemaliza mafunzo ya kiitikadi na mbinu huko Rumangabo mjini Goma chini ya AFC/M23. Sasa wakiwa na vifaa kamili na wanaolipwa, wametumwa Lubero, ambako wanashiriki kikamilifu muungano wa serikali."
Wakati huo huo, Uganda imetangaza kuwa vikosi vyake vya kijeshi vimeanza kuelekea Bunia, DRC, ikiwa ni siku chache baada ya Jeshi la Uganda kutoa muda wa saa 24 kwa askari waliopo eneo hilo kujisalimisha.
Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi wa Uganda (CDF) alichapisha ujumbe mfupi kwenye mtandao wa X uliosema, "Bunia... Wachwezi wana kuja," na baadaye akaongeza, "Turaza kabisa," akisisitiza kuwa vikosi vyao vinaingia rasmi ndani ya mji huo.
Mzozo Mashariki mwa DRC umeendelea kuzua taharuki, huku mapigano yakiongezeka na mataifa jirani kama Uganda na Rwanda yakitajwa kuwa na ushawishi mkubwa katika hali inayoendelea. Serikali ya DRC imesisitiza kuwa itaendelea kupambana dhidi ya waasi wa M23 na washirika wao, ikitafuta msaada wa kimataifa kuimarisha ulinzi wake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED