Aweso aitaka DAWASA kushirikiana kwa karibu na wenyeviti wa mitaa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:48 PM Feb 18 2025
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kushirikiana kwa karibu na wenyeviti wa mitaa ili kuweza kutatua changamoto za maji pamoja na kurahisisha ufikishaji wa huduma zinazotolewa na mamlaka hiyo.

Aweso ameyasema hayo leo Februari 18, akizungumza na Wenyeviti wa Mitaa wa Wilaya ya Kinondoni na kusema kuwa “Niwaombe sana Wenyeviti wa mitaa tuwape ushirikiano DAWASA na pia niwaombe DAWASA muwape ushirikiano Wenyeviti”

Aweso amewataka viongozi wa mamlaka hiyo kuhakikisha kila wakati wanashiriki mikutano inayofanywa na wenyeviti hao ili kuweza kusikiliza na kutatua changamoto zilizopo katika maeneo yao.

“Muwape ushirikiano muwe na mawasiliano yao wakipiga simu muwape taarifa wakiwaita wana mkutano mtu wa maji awepo naomba sana mtu wa DAWASA awepo asikilize muweze kutatua changamoto zilizopo kwenye hayo maeneo”

1

Aidha Aweso ameitaka mamlaka hiyo kuwa na utaratibu wa kutoa taarifa za haraka hasa za hitilafu na matengenezo ili kuepuka kutokea kwa sintofahamu na upotoshaji wa taarifa.

“Wakati mwingine zipo hitilafu zinajitokeza niwasihi sana zinapotokea hitilafu viongozi wasione hitilafu kwenye mitandao wapeni taarifa wenyeviti” 

Pamoja na hayo Waziri Aweso ameipongeza DAWASA kuwa wa kwanza kutekeleza agizo alilotoa la kuwataka viongozi wa mamlaka za maji nchini kukutana na Wenyeviti wa mitaa na kushirikiana nao ili kutatua changamoto cha maji na kutekeleza miradi ya maji nchini.