TANZANIA na Misri, zimejadiliana namna bora ya kushirikiana katika kukuza na kuendeleza utalii kati ya nchi hizo mbili.
Hayo yamejiri leo, Februari 18, 2025 jijini Dar es Salaam katika kikao kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi, Dk. Pindi Chana na Balozi wa Misri nchini Tanzania, Sherif Abdelhamid Ismail.
“Nchi zetu zinafurahia uhusiano wa kidiplomasia wa muda mrefu na wenye manufaa, ambao tunaamini unaweza kuwa ushirikiano thabiti katika Sekta ya utalii pia.”
Chana amesisitiza huku akifafanua kuwa Tanzania inatamani kuongeza idadi ya watalii kutoka nchini Misri na kuvutia wawekezaji kuangalia fursa mbalimbali za utalii zinazopatikana nchini Tanzania.
“Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa mazao ya utalii ikijumuisha katika eneo la huduma ya malazi, usafirishaji, mashirika ya ndege, shughuli za utalii, vifaa vya mikutano,uwindaji wa kitalii na kisiwa kizuri katika Bahari ya Hindi, kinachofaa kabisa kwa uwekezaji” alisema Chana.
Kwa upande wake Balozi wa Misri nchini, Mhe. Sherif Abdelhamid Ismail, alisisitiza kuwa kwa wingi na upekee wa vivutio ilivyonavyo, Tanzania ina uwezo wa kuvutia zaidi ya watalii milioni 10 kwa mwaka, na ofisi yake iko tayari kushirikiana na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika kuendeleza na kutangaza utalii nchini.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Makumbusho ya Taifa la Tanzania (NMT), Wizara ya Maliasili na Utalii na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED