Maprofesa watangaza dawa ya kudhibiti udanganyifu mitihani

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:01 AM Jul 05 2024
Makamu Mkuu Chuo Kikuu Huria Tanzaia, Prof. Elifasi Bisanda.
Picha: Mtandao
Makamu Mkuu Chuo Kikuu Huria Tanzaia, Prof. Elifasi Bisanda.

MAPROFESA wa vyuo vikuu mbalimbali nchini wamependekeza njia za kudhibiti udanganyifu wa mitihani elimu za juu, kwa kuondoa utaratibu wa kuajiri kwa kutegemea vyeti pekee bali uelewa wakati wa usaili.

Aidha, wamependekeza kuwe na mfumo wa kumtambua mtahiniwa kwa alama za vidole kabla ya kuingia kwenye chumba cha mtihani, ili kuziba mianya ya wanaotoa fedha kufanyiwa mitihani.

Maprofesa hao walitoa mapendekezo hayo juzi katika kipindi cha mizani kinachorushwa na TBC kilichokuwa na mada ya ‘Udanganyifu wa mitihani elimu ya juu’.

Makamu Mkuu Chuo Kikuu Huria Tanzaia, Prof. Elifasi Bisanda, alisema kupima uelewa kwa kutumia cheti ni njia inayochangia udanganyifu, ndio maana wanafunzi hupambana kwa njia haramu kupata vyeti na sio kuelimika.

Alitoa mfano wa Marekani ambayo imeshavuka hatua ya kumpima mtu kwa mtihani au cheti badala yake wanampima kwa kumhoji mpaka wanagundua kama atafaa kutumikia nafasi fulani au la.

“Tunahangaika bure mitihani sio kigezo halisi cha kupima uelewa wa mtu, fikiria unasoma mwaka mzima halafu unafanya mtihani kwa saa mbili unawezaje kutumia elimu ya mwaka mzima kuielezea kwa saa mbili?

“Tumekuwa wavivu kutafuta mbinu mbadala za kupima uelewa, nchi kama Marekani hawaangalii vyeti tofauti na huku, kule wenzetu wanakuhoji wanakuchunguza wanapokuhoji wanajua una uwezo kiasi na unaweza kuwafanyia kazi.

“Dhana ya mitihani kama ndio kigezo cha ubora wa elimu naielewa, lakini angalia mfano nchi kama Finland, ndio wanaoongoza kwa ubora wa elimu, lakini mtoto akianza darasa la kwanza hafanyi mtihani mpaka akifikisha miaka 16 ndio anafanya wa kuingia chuo kikuu na wote wanafaulu.

“Lakini elimu yetu kuanzia darasa la kwanza ni mitihani tu, Ninachofikiri wana taaluma tujikite katika kubuni namna gani ya kupima uelewa nje na kufanya mtihani.

Prof. Bisanda alifafanua namna aliowaita mamluki 17 kuingia katika chuo chake na kuwafanyia mtihani baadhi ya wanafunzi katika chuo hicho akibainisha kuwa walitumia njia ya kughushi vitambulisho.

“Baada ya kuwa tumebana kila njia ya udanganyifu, imeibuka hii mbinu ya kutafuta ‘mamluki’ wanakuja kufanya mtihani ukaanza huo ujanja, lakini kwa bahati nzuri tumekuwa macho wale wasimamzi walisaidia tukawanasa.

“Lilitokea wiki mbili watu waliingia kufanya mtihani wakati wanaingia walikuwa wana vitambulisho vya aina mbili cha chuo na cha kufanyia mtihani ambacho kinapicha yake na ratiba ya masomo anayotakiwa kufanyia mtihani.

“Inavyoonekana wale walifoji vitambulisho, kwa hiyo kuna mtu mmoja kwa mfano alikuwa anaenda kumfanyia msichana, lakini kitambulisho cha mvulana jina ni la kike kwa huyo ilikuwa rahisi kumtambua kwamba wewe unaenda kufanya mtihani wa Rabeka wakati wewe ni Hassan haiwezekani,” alibainisha.  

Alisema walikuwapo wengine walitumia vitambulisho vinavyoonekana kama halali kumbe yale maandishi ya juu yalikuwa makubwa sasa wale wasimamizi walipoona vile hawakuwazuia kufanya mtihani utaratibu wetu ni muache kwanza tuone anataka kufanya nini.

Prof. Bisanda alisema walipoanza kufanya mtihani wakaguzi walipita kila dawati kukagua walipowafikia walibiani vitambulisho vyao vina shaka na kwamba kosa walilofanya ni la jinai watashughulikiwa na vyombo vya usalama kwa mujibu wa sheria za nchi.

Alisema kipindi cha nyuma walilazimika kuondoa mitihani katika mikono ya walimu kwa kuwa wengi walihusika kuvujisha mitihani na kwamba kwa sasa wana mfumo unaoziba mwanya huo.

Katika kupambana na udanganyifu wa mitihani katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Mhadhiri Mwandamizi wa Shule Kuu ya Elimu, Dk. Eugenia Kafanabo alisema wanakitengo cha udhibiti ubora kinachosimamia mfumo mzima wa ufundishaji kutoka utungaji wa mitihani, usahihishaji mpaka matokeo.

“Sio kwamba UDSM hatukosei, hapana wengi ambao wanakuwa na vitambulisho feki wanatengeneza mtaani kwa sababu hawajalipa ada, anakwenda kutengeneza ili aonekane ni mwanafunzi halali ilimradi afanye mtihani na wengine ndio kama hivyo wanatuma mamluki waje kuwafanyia mtihani.

“Kwahiyo siku hizi mwanafunzi anapokusanya mtihani tunalinganisha na kitambulisho chake kama namba ya mtihani aliyoandika inafanana na ya kwenye kitambulisho chake na wengi wanakamatwa kwa huu mfumo,” alisema Dk. Eugenia.  

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Taaluma Utafiti na Ushauri Elekezi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Prof. Razaki lokina, alisema udanganyifu upo katika ngazi zote za elimu.

“Udanganyifu wa mitihani ni vitu ambavyo vinafanana katika kila chuo, suala la vitambulisho tunajaribu kuona namna gani tunaweza kutumia mfumo wa sura ya mtahiniwa iwekwe katika mfumo,” alisema.  

Mtafiti wa Utahini na Udanganyifu Kwenye Mitihani, Dk. Setini Kita, alizitaja njia zinazotumika kwenye udanganyifu kuwa ni pamoja na kuingia na vikaratasi, kujiandika katika miili yao, kutumia majibu bila wasimamizi kujua, wafanyakazi kuvujisha mitihani, na kutumia simu.

WANAFUZI

Mwanafunzi wa UDSM, Diniel Safar, akizungumzia udanganyifu wa mitihani alisema tabia hiyo inasababisha madhara kwa wasio na tabia hiyo kwa kuwa watashawishika kuingia kwenye mkumbo huo.

Mwanafunzi Rose Ngalo, alisema mpaka inatokea mwanafunzi anafanya udanganyifu huo maana yake kuna baadhi ya walimu wamehusika kwa namna moja ama nyingine.

“Mara nyingi huwa yanakuwa mazingira ya rushwa, hivyo ni bora kuwe na uaminifu kwa wanafunzi na walimu,” alisema.