Kikwete aifagilia REA kusambaza umeme vijiji 12,031

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 12:20 PM Jul 08 2024
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, akipewa maelekezo kuhusu matumizi ya jiko lenye sufuria ya kupikia kwa kutumia nishati ya umeme (pressure Cooker) kutoka kwa watumishi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) jana katika Maonesho ya Sabasaba
PICMPIGAPICHA WETU
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete, akipewa maelekezo kuhusu matumizi ya jiko lenye sufuria ya kupikia kwa kutumia nishati ya umeme (pressure Cooker) kutoka kwa watumishi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA) jana katika Maonesho ya Sabasaba

RAIS Mstafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amewapongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kusambaza nishati ya umeme kwa vijijiji 12,031 na kuongeza kuwa wakati akiwa anaondoka madarakani mwaka 2015 umeme ulikuwa umefika kwenye vijiji 2,000 tu.

Dk. Kikwete ametoa pongezi hizo jana alipotembelea banda la REA kwenye Maonesho ya 48 ya Kimatifa ya  Biashara ya Dar es Salaam (DITF); yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba, barabara ya Kilwa, mkoani Dar es Salaam.

Rais Mstaafu Kikwete amepongeza kazi kubwa ya kusambaza nishati ya umeme vijijini na kusema wakati anaingia madarakani mwaka 2005 ni asilimia 4 tu ya wananchi wa vijijini ndio walikuwa wamefikiwa na nishati ya umeme.

“Leo zaidi ya vijiji 12,031 vimeunganishwa na umeme, ni zaidi ya asilimia 98, vilivyobaki ni vijijini 207 tu,” alisema Dkt. Kikwete.

Alisema kwa idadi hiyo ni wazi kuwa wananchi wengi wa vijijini wameunganishwa na umeme na hivyo kufanya watumiaji wa umeme nchini kuongezeka.
Amesema  iwapo bei ya umeme itapungua, itawafanya wananchi wengi zaidi kutumia nishati hiyo kwa kupikia kwa sababu kuna majiko ya umeme yanayotumia umeme kidogo.

WhatsApp Image 2024-07-08 at 11.41.03 AM (1).jpeg 105.9 KB


“Tuangalie TANESCO wasipandishe bei ya umeme; wananchi wengi wataweza kuutumia umeme kama nishati safi ya kupikia, sasa hivi mkaa na kuni ndio wapinzani wakubwa wa umeme. Miti inakatwa kweli kweli, tunaharibu mazingira, na hatupandi miti kwa kasi ile ile,” amesema Dk. Kikwete.

Alitoa mfano kuwa miaka kadhaa iliyopita akiwa nyumbani kwake Msoga, mkoani Pwani, alikuwa hawezi kuona hata magari yakipita Chalinze kwa sababu ya misitu ya miti, lakini sasa anaweza hata kuhesabu idadi ya magari yanayopita Chalinze akiwa Msoga na kuwa misitu imebaki tu kwenye makaburi.

“Matumizi ya mkaa ni makubwa, miti inakatwa sana, tupunguze matumizi ya mkaa na kuni lakini pia tupande miti na tutumie nishati safi yakiwemo majiko banifu, lakini bei ya umeme iangaliwe na ipungue ili Wananchi wengi waitumie,” Amesisitiza Dk. Kikwete.

Aidha, amewataka wauzaji wa gesi ya kupikia wasiwe na tamaa kupandisha bei ili wananchi wengi wahamasike kuitumia katika kupikia.