KASI NDOA KUVUNJIKA: Mchawi mkuu huyu hapa; ndoa moja…

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:56 PM Jul 08 2024
Mchoro wa maharusi ambapo kwa mujibu wa utafiti NBS, inaonesha asilimia 57 ya Watanzania hawako katika ndoa.
Picha: Maktaba
Mchoro wa maharusi ambapo kwa mujibu wa utafiti NBS, inaonesha asilimia 57 ya Watanzania hawako katika ndoa.

RIPOTI ya Utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) 2020/21 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonesha asilimia 57 ya Watanzania hawako katika ndoa.

Hata asilimia 43 ya walio katika ndoa nao wanakabiliwa na balaa. Shida kuu ni kwamba 'taasisi ndoa’ imetikiswa.

Wataalamu wa saikolojia na wahadhiri wameeleza kiini cha wanandoa kutodumu, wakinyooshea kidole malezi duni kwa watoto kwa kizazi cha sasa na ukuaji wa teknolojia kuwa ndiyo mzizi wa tatizo.

Wamesema zipo athari katika maisha yao baadaye ukubwani hasa katika ndoa au uhusiano, kwamba wanapokumbana na changamoto wanazikabili na si kurudi kwa mama au baba kupata maelekezo.

Msaikolojia Tiba wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dk. Isaac Lema, anasema kuwa hivi sasa ni kawaida kwa mtu mzima (mwenye umri wa kuanzia miaka 18) mwenye familia, akiwa na changamoto za kifamilia hasa wanandoa kurudi kwa mzazi kuchukua maelekezo badala ya ushauri.

“Unakuta mtu ana kisa na yuko katika ndoa, anampigia simu mama yake, tunataka tununue gari wewe unasemaje? Unakuta kijana huyu kujitegemea katika uamuzi wake ni tatizo. “Kila umri una rasilimali unazohitaji, ukimpa mtoto rasilimali maarifa kulingana na umri wake maana yake umemsaidia,” alisema Dk. Lema.

Alisema kuna pengo kati ya malezi na jamii, huku familia ikiachiwa jukumu hilo pekee, wakati   familia   hizo hivi sasa nazo zinaandamwa na changamoto za kutafuta maisha zaidi.

“Kazi ni kile kinachozalishwa kuliko muda unaotumika kwenye kazi yenyewe. Kila hatua ya malezi inamsaidia mtoto kujitegemea, ili afikapo miaka zaidi ya 18 aweze kujitegemea.”

“Malezi yanahitaji muda, kuji- toa, mpangilio, kupanga ni kuchagua. Uangalie kazi ya mwajiri, lakini pia malezi, maisha ya kila siku. Kama una majukumu ya kikazi pia utenge muda wa malezi, ni sehemu ya kazi zako za kila siku.”

“Unapokuwa nyumbani unapika, kwanini usimshirikishe mtoto aje karibu umwelekeze namna  ya  kupika? Unapokwenda kwenye mazoezi kwanini usiende naye ajifunze?”  Dk. Lema anasema.

Mtaalamu huyo anasema mtoto anapohusishwa katika shughuli tofauti pamoja na mzazi au mlezi, inaongeza utamaduni wa kuwasilisha jambo na changamoto anazokumbana nazo.

“Mtoto akiweza kujitegemea ndivyo unavyopata muda na wewe wa kufanya kazi zingine. Malezi ni kazi, kazi ya mwajiri unaweza kupeleka nyumbani lakini kazi ya malezi huwezi kupeleka kazini.

“Mtoto lazima awe na mipaka. Mtoto ili  asisumbue unampa simu kama namna ya kumdhibiti, ili  asikusumbue badala ya kumhusisha kile unachokifanya, anajifunza taratibu,” alifafanua.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Dk. Jabhera Matogoro, anasema kipindi cha likizo kwa watoto ni muda mzuri kwa wazazi na walezi ku- zungumza nao ikiwamo kuwapa muda wa wao kutoa maoni.

“Ni kweli tuko ‘bize’ ila lazima kuweka uwiano katika maisha. Tunapotenga muda wa kuzungumza na vijana inasaidia kujua ukuaji wao.

“Katika dunia iliyojaa majukumu na teknolojia, lazima hatua hii ichukuliwe ili kukupa muda kufahamu familia na ukuaji wa akili na kuchukua hatua kwa wakati sahihi."

“Nilihudhuria mjadala UDOM, mwasilishaji mada akazungumza kwamba malezi yanaweza    kuchangia ama kuathiri ukuaji wa mtoto.

“Matumizi ya teknolojia yanaongeza familia kujitenga, huku baba akiwa na chombo chake cha   mawasiliano, yaani simu, mama na mtoto hivyo hivyo, jambo hili linasababisha kuwapo wigo   miongoni mwao.

“Utakuta mtu ameingia katika uhusiano mpya ama  ndoa, ikafika wakati kukawa na tofauti na uhusiano huo ukakoma, utakuta  mmoja  alikuwa  na  picha, uhusiano  unapokoma  anaanza kuziachia picha ambazo mlipiga awali,  hii  ina  athari,  teknolojia inaathiri,” anasema Dk. Matogoro.

Anasema majukumu ya kikazi yasiwe kikwazo kwa familia kujitenga katika malezi, akisema teknolojia itumike kumhusisha mwanafamilia kama baba au mama, aliye mbali na upeo wa macho yao, kwa kuungana kupi- tia teknolojia ya mawasiliano ili kukuza ukaribu.

Agness Andrew (56), mkazi wa Mwananyamala, mkoani Dar es Salaam, anasema wazazi kutoa   maelekezo kwa watoto wao baada ya kuona au kuolewa hutokana na sababu nyingi.

“Malezi ya siku hizi mengi yanaegemea kwetu kinamama…umelea watoto wako pengine baba    wala hakutoa mchango wowote. Watoto wanaona, mama nimehangaika kuwasomesha, baadaye huwa na uchungu na kuniamini sana mama yao.

“Mimi nilimwambia kijana wangu akioa awe na mke mwenye heshima na kupenda wazazi wa pande zote mbili. Siyo mwanangu kaoa, mwanamke ndipo anampanda kichwani. Hata mimi   huku   ananisahau, nani atavumilia?” Agness anahoji.

Kwa mujibu wa ripoti tajwa ya NBS, wanandoa waliotengana nchini ni asilimia tano, waliopeana talaka ni asilimia 1.9, wasiowahi kuwa katika ndoa ni asilimia 38.9, wajane na wagane ni asilimia 5.4 na wanaoishi kiu- chumba ni asilimia 6.1.

Utafiti huo wa NBS pia unaonesha  kuwa  idadi  ya  wasioishi  katika  ndoa vijijini  ni  asilimia  55.5  ya  waliofikia  umri  wa kuoa au kuolewa, huku mijini ni asilimia  61.5  sawa  na  tofauti  ya asilimia sita.

Kwa mujibu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), kwa mwaka 2019 talaka nchini zilikuwa 442, mwaka 2020 ulikuwa na talaka 511 na mwaka 2021 zilikuwa 550.

Takwimu za RITA zinaonesha kuwa mwaka 2019, ndoa 43,479 zilisajiliwa huku mwaka 2020, zikisajiliwa ndoa 54,071, mwaka 2021 ndoa 49,000 na mwaka 2022 ndoa 51,011.

Vilevile, takwimu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum zinaonesha   kulikuwa na migogoro ya ndoa 39,571 katika kipindi cha kuanzia Julai 2021 hadi Aprili 2022. Kati yake, migogoro 19,262 ilipata suluhu, 15,718 ilikuwa katika usuluhishi na 4,576 ilikuwa mahakamani."

Utaratibu wa kisheria unaelekeza kukishakuwa na  mgogoro katika ndoa, wanandoa wanapaswa kuanzia kwa Ofisa Ustawi wa Jamii ambako ikishindikana, ndiko hupewa baraka za kufikisha mgogoro huo mahakamani.