CCM yaweka imani kwa wananchi ushindi wa kishindo uchaguzi ujao

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 04:08 PM Jul 08 2024
Katibu wa NEC, Siasa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla (wapili kulia) akikagua moja ya miradi.
Phich: Romana Mallya
Katibu wa NEC, Siasa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla (wapili kulia) akikagua moja ya miradi.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kazi kubwa iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kupeleka fedha za miradi katika maeneo tofauti ni ushindi tosha kwa chama hicho uchaguzi ujao.

Katibu wa NEC, Siasa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, amesema hayo leo wakati alitembelea miradi katika sekta ya elimu na afya inayotekelezwa na serikali.

Katika ziara yake ya siku saba, Makalla leo ametembelea Shule ya Sekondari ya Minazi Mirefu iliyoko jimbo la Ukonga inayoendelea na ujenzi na Kituo cha Afya Kinyerezi.

"Tumekuja kuona jitihada za serikali na kazi kubwa iliyofanyika ya kuboresha huduma kwa wananchi wetu wa kata hii ya Kinyerezi na Jimbo la Segerea wote ni mashahidi tunaposema maendeleo yanaonekana sio kwa tochi kama tunavyoona majengo makubwa ya Kituo cha Afya cha Kinyerezi.

"Kwa wasio amini waje wapate huduma maana ni maendeleo makubwa, ndio maana tunampongeza Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wetu,  Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha huduma.

Amesema kwa  huduma wanazoziona hapo ikiwamo vipimo vya kisasa vinavyohudumia wagonjwa ni dhahiri kuwa serikali imedhamiria kwa dhati kuwahudumia wananchi wake.

"Magonjwa yote, operesheni ndogo ndogo zinafanyika,wodi za wazazi nzuri tumeona kliniki zinavyoendelea na wagonjwa wanavyopata huduma hapa. Kwa kweli Kituo Cha Afya Kinyerezi kimekuwa msaada mkubwa sana," amesema.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Zaituni Hamza, kituo hicho mwaka 1976 kilianza kama zahanati  na baadaye kiliongezewa majengo na kupandishwa hadhi.

Amesema kwa sasa kinatoa huduma kwa wananchi zaidi ya 200,000 kikihudumia mitaa sita.

Amina Yahya, mwananchi wa Kinyerezi aliyekutwa kituoni hapo akisubiri kupatiwa huduma, amesema kupandishwa hadhi kutoka zahanati hadi kuwa kituo, kumechangia wananchi kupata huduma zenye hadhi.

"Tunashukuru serikali kwa hatua hii ambayo ina maana kubwa kwa wananchi kwa kuwa kama unafika hapa unapata huduma muhimu ni jambo kupongeza,"amesema.