Yatima Kibaha wakumbukwa, wafanya dua kumwombea Rais Samia

By Yasmine Protace , Nipashe
Published at 02:26 PM Jul 08 2024
Yatima Kibaha wakumbukwa, wafanya dua kumwombea Rais Samia
Picha:Mpigapicha Wetu
Yatima Kibaha wakumbukwa, wafanya dua kumwombea Rais Samia

VITUO tisa vya kulea watoto yatima katika Mji wa Kibaha mkoani Pwani,vimeungana na viongozi wa dini na serikali kwa kufanya dua maalumu kwa kumuombea Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kutokana na kuwaletea maendeleo makubwa toka aingie madarakani.

Dua hiyo,imefanyika katika viwanja vya kituo cha Shallom,kilichopo Mkuza kwa watoto wa vituo hivyo kupewa msaada mbalimbali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mji Kibaha Dk.rogers Shemelekwa alisema kuwa baada ya kumaliza mwaka wa fedha,watumishi walitafakari  na kuona kuna hali ya kuwasaidia watoto wenye uhitaji.

Alisema katika kuyafikia malengo hayo,ndipo watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha kwa kushirikiana na Watumishi wa Shirika la Elimu Kibaha pamoja na wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya CRDB wametoa vifaa mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 4.2 kwa makao tisa ya vituo vya kulea watoto yatima.

Shemwelekwa alisema kuwa wao na watoto hao ni familia moja hivyo wameamua kuwasaidia ili kuwapa faraja na amani hivyo wasijione wapweke na hakuna yatima na serikali inapenda watoto ndiyo sababu ikaweka elimu bure ili watoto wapate haki ya msingi ya kupata elimu.

"Serikali inawapenda na ndio maana ikaamua kutoa elimu bure kuanzia elimu ya awali hadi Sekondari," alisema.

1

Aliongeza kuwa "Watoto hawa wanahitaji sukari, madaftari na mahitaji mengine na tukiwasaidia tunaweka hazina mbinguni na sisi tutaendelea kuwasaidia,"alisema Shemwelekwa.

Akizungumzia miaka mitatu ya mama Samia katika wilaya yao,alisema kuwa kupitia miaka mitatu ya Dk.Samia amewafanyia Mambo majubwa ya kimaendeleo.

Mwakilishi wa Mbunge wa Mji wa Kibaha,Joseph Jackson alisema mkurugenzi alichokifanya hakijawahi kutokea katika mkoa wa Pwani.

" Ninamiaka zaidi ya 20,sijawahi kukiona hiki kitu kufanywa na wakurugenzi hivyo naona wakurugenzi wengine wanatakiwa kuyaiga haya," alisema.

Aliongeza kuwa kuwajali watoto yatima kunasaidia watoto hao kuishi kwa furaha.

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba amesema kuwa anapongeza wadau waliofanikisha kupatikana kwa misaada hiyo.

Mussa amesema kuwa wamejikita katika kuhakikisha watoto hao wanapata elimu kama ilivyo kwa watoto wanaoishi na familia zao kwani elimu ni haki yao.
2

Jamila Juma kutoka kituo cha Shallom alisema kuwa anawashukuru wote waliojitoa na kuwasaidia mahitaji ya shule ikiwamo kuwakutanisha na watu mbalimbali kwao ni faraja tosha.

" Watoto yatima tunapitia changamoto nyingi,majumbani na ndio maana tunalelewa vituoni,lakini tunawashukuru wote kwa kutujali kwa misaada yao," alisema.

Kwa upande wake Ofisa Ustawi wa Jamii Faustina Kayombo amesema kuwa Halmashauri ina makao tisa yenye watoto 601 na yote yamesajiliwa kisheria na kwa upande wa mafanikio ni makao kuwa na majengo bora.

Kayombo amesema kuwa changamoto ya watoto kuishi kwenye mazingira magumu ni pamoja na kubakwa, wazazi kupoteza upendo, mahusiano mabaya na wazazi.

Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na mahitaji ya shule, magodoro, madaftari, kalamu, penseli, vichongeo, rula, mafuta ya kujipaka, mafuta ya watu wenye ualbino na taulo za watoto wa kike.


Sherehe hizo zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Madiwani wa Halmashauri, wazee maarufu, viongozi wa dini, makundi mbalimbali yanayomuunga mkono Rais, vikundi vya sanaa na wananchi.

3