TET, Educate washirikiana kunoa walimu masomo ya biashara

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:21 PM Jul 08 2024
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Aneth Komba, kushoto, kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Educate Kamanda Kamiri. Picha Maulid Mmbaga.
PICHA: MAULID MMBAGA
Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Aneth Komba, kushoto, kulia ni Mkurugenzi wa Shirika la Educate Kamanda Kamiri. Picha Maulid Mmbaga.

TAASISI ya Elimu Tanzania (TET) na Shirika la Educate wameingia makubaliano ya miaka sita kwaajili ya kutoa elimu ya mafunzo endelevu kwa walimu wa masomo ya biashara, ikiwa ni mojawapo ya hatua za utekelezaji wa mtaala mpya ulioboreshwa.

Akizungumza leo mkoani Da es Salaam, Mkurugenzi wa TET Dk. Aneth Komba amesema makubalino hayo pia yanalenga kuwawezesha walimu kufundisha somo la biashara kwa kutumia mbinu za kisasa na kuwa na maarifa yanayoendana na wakati katika ufundishaji.

Amesema makubaliano hayo yanalenga pia kuwezesha TET kuwa kitivo cha utafiti utakaosaidia kukuza na kubadilishana uzoefu na ujuzi katika utekelezaji wa mafunzo ya somo la biashara, pamoja na kumuandaa mtanzania anaeweza kushindana kimataifa.

"Niwaombe walimu ngazi ya sekondari watengeneze jumuia za ujifunzaji na wajifunze kupitia matini mbalimbali ambayo yako kwenye mfumo wa 'learning management system' ambao unapatikana bure," amesema Dk Aneth.

Ameongeza kuwa wameanzisha rasmi programu ya kuajiri walimu wa kujitolea kwa somo la biashara katika shule zitakazoainishwa kwamba zinauhitaji mkubwa ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu wa somo husika, wakati wa utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa.

WhatsApp Image 2024-07-08 at 4.04.39 PM.jpeg 81.58 KB
Amesema programu hiyo ni sehemu ya makubaliano hayo ambayo yatasaidia pia kuajiri walimu kwa mkataba katika shule zenye uhitaji.

Aidha, amebainisha kuwa mtaala mpya ulioboreshwa umeanza utekelezaji wake rasmi mwezi huu kwa kidato cha tano na elimu ya ualimu Stashahada, na kwamba TET wamejipanga vizuri kuhakikisha maandalizi ya kutoa mafunzo kwa walimu pamoja na vifaa vya ufundishaji vinakuwepo.

Mkurugenzi wa Shirika la Educate, Kamanda Kamiri, amesema tangu 2022 katika awamu ya kwanza ya ushirikiano walipata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mtaala, na kwasasa wamesaini makubaliano pia ili kuendeleza pale walipoishia.

"Lengo letu ni kuhakikisha kwamba tunawandaa watoto kukabiliana na maisha baada ya kuhitimu, kwa kuwapatia maudhui mazuri yanayoendana na dunia ya sasa , tumeshamaliza awamu ya kwanza sasa tuko katika awamu ya pili, ikiwemo kutoa elimu kwa wakimu," amesema Kamiri.