Kikundi chaanzisha huduma kusaidia mabinti,wanawake wanaopitia changamoto

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 04:37 PM Jul 08 2024
Kikundi chaanzisha huduma kusaidia mabinti,wanawake wanaopitia changamoto
Picha: Mpigapicha Wetu
Kikundi chaanzisha huduma kusaidia mabinti,wanawake wanaopitia changamoto

KIKUNDI cha Huduma ya Matumaini Mapya, kimeanzisha huduma ya kufundisha neno la Mungu, kuwashauri mabinti na wanawake wanaopitia changamoto mbalimbali za maisha kusimama imara ili kutimiza ndoto zao.

Uamuzi wa kuanzisha kikundi hicho, umetokana na baadhi ya wanawake na mabinti kukata tamaa wanapoteswa kwenye mahusiano, ndoa, madeni na magonjwa  na kusababisha kuishi maisha ya majuto na mawazo hali inayohatarisha kupata magonjwa ya afya ya akili.

Mwenyekiti wa Kikundi hicho, Theresia Kibona akizungumza jana na waandishi wa habari, amesema wameanzisha kikundi hicho mwaka 2023 mahsusi kuwasaidia wanawake waliokata tamaa ya maisha kiroho na kimwili kupata matumaini mapya na kusonga mbele.

Amesema katika kuhakikisha hayo yanafanikiwa, wameweka utaratibu wa kukutana kila mara kujifunza neno la Mungu, kupeana ushauri  wa nmna ya kujikwamua kiuchumi.

“ Namshukuru Mungu amenipa kibali cha kumtumikia na kukutana na watu mbalimbali waliokata tamaa kwenye maisha, nimekuwa mshauri wao kiroho na kimwili  hadi wanafanikiwa kuvuka kwenye magumu yao, tumekuwa tukitoa msaada wa hali na mali kwa watu wasiojiweza  zikiwemo nyumba za ibada,” amesema Theresia.

1

Katika Ibada ya shukrani na kumbukizi ya kuzaliwa kwake, Theresia akiwa na wanachama wenzake,  wametoa msaada wa viti katika  kanisa la Elbethel Pentecostal Church for all Nations,  lilipo Kivule kwa Majohe na Kupunguni jijini Dar es Salaam.

Msaada huo unetokana na michango iliyotolewa na wanachama wa kikundi cha Matumaini mapya ambao wengi wao ni wafanyabiashara wa soko kuu la Kimataifa Kariakoo.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi, Suzana Kimambo amesema wametoa msaada wa viti 120 vyenye thamani ya sh. milioni 8.4 pamoja na zawadi nyingine kwa wajane na watoto yatima kanisani hapo.

Katibu wa Kikundi hicho, Loveness Kibona, amesema walianza huduma wakiwa watu 12 na kwamba hadi sasa wamefikia 40, malengo yao ni kuhakikisha wanakuwa sehemu salama ya watu kupata huduma ya neno la Mungu na kupata ushauri nasaha kukabiliana na changamoto za maisha.
2

Ameongeza wamepanga kuendelea kuisaidia jamii kuwa kuyafikia makundi yote yenye mahitaji kama walivyofanya mwaka 2023 kwa kukitembea kituo cha waraibu wa  dawa za kulevya, kilichopo Pugu ambapo walitoa misaada wa mavazi, chakula na mahitaji mengine.

Akipokea msaada huo Mchungaji wa Kanisa la Elbethel Pentecostal Church, Raphael Mhagama, amewashukuru wanakikundi kwa msaada huo kwa madai walikuwa na uhaba wa viti na tayari walianza kuchangishana ili kuvinunua.

Amesema msaada huo ni muujiza kwao kwani hawakutegemea na kwamba wameweka alama kwa kanisa, kila siku wataendelea kuwaombea ili wabarikiwe kimwili na kiroho kupitia sadaka hiyo walizozitoa kanisani hapo.
3