Korti yatoa amri wanaodaiwa kuwa ‘dadapoa’ wakamatwe

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 07:31 AM Jul 05 2024
Washtakiwa wanaodaiwa kuwa makahaba wakiwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive (Jiji).
Picha:Mtandao
Washtakiwa wanaodaiwa kuwa makahaba wakiwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive (Jiji).

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive (Jiji) imetoa amri ya kukamatwa kwa kinadada watano kati ya 18 katika kesi ya kufanya vitendo visivyo vya heshima maeneo ya umma na kuvaa mavazi yasiyokubalika kwa nia ya kufanya ukahaba, kwa kushindwa kufika mahakamani bila taarifa.

Amri hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Lugano Kasebele wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na Amina Ramadhani, Aisha Iddi, Mariana Sia, Mwajuma Hamza, Mariamu Hassan, Najma Hamisi, Sabrina Gabriel, Mariam Kitamoga, Elizabeth Michael.

Wengine ni Rosemary John, Recho Kindole, Lobi Daudi, Diana David, Jackline Daniel, Mwajuma Bakari, Jenifa John, Zainabu Hamisi na Recho Bakari.

Hakimu Kasebele alifikia uamuzi huo baada ya Wakili wa Serikali Regina Kayuni kuita majina ili kujua kuwapo kwa washtakiwa mahakamani huko na kubaini kuwa watano hawakuhudhuria. Hao ni mshtakiwa namba mbili, saba, 11, 13 na 17.

"Kitendo hiki ni kutokuheshimu na kutotii amri ya mahakama na kuwa washtakiwa wanataka kufanya tabia hiyo kuwa ni mazoea.

"Ninatoa amri ya kukamatwa kwa washtakiwa kwa kushindwa kutii amri ya mahakama," alisema Hakimu Kasebele. 

Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Peter Madeleka alidai kuwa mahakama inaweza kuchukua hatua dhidi yao ili iwe funzo kwa wengine watakaoonesha kutotii na kutofuata amri ya mahakama; haijalishi huyo mtu ni nani na ana nafasi gani katika jamii.

"Tumewaelekeza wateja wetu namna ya kutii na kufuata amri ya mahakama kwa jinsi tulivyoweza. 

"Kama mahakama inaona wamevunja sheria, basi ichukue hatua dhidi yao na wakamatwe," alidai Wakili Madeleka.

Hakimu Kasebele alitoa amri ya kukakatwa kwa washtakiwa hao watano ili iwe funzo kwa wengine watakaokiuka na kuacha kutii amri ya mahakama kama inavyowaelekeza.

Alisema kuwa kesi imepangwa kusikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi, Francis Mhina. Kesi hiyo iliahirishwa hadi hadi Julai 10 mwaka huu kwa ajili ya washtakiwa kusomwa hoja za awali.

Katika kesi hiyo, inadaiwa kuwa Juni 14 mwaka huu, katika maeneo ya Sinza Mori, wilayani Ubungo, Dar es Salaam, washtakiwa wote 18 walikutwa wanajiweka katika namna ambayo siyo sawa mbele za umma na kufanya vitendo visivyofaa na kuvaa mavazi yasiyokubalika kwa nia ya kufanya ukahaba.