Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche, amesema licha ya Tanzania kuwa na rasilimali nyingi, bado Watanzania wengi wanashindwa kumudu gharama za maisha.
Akizungumza na wananchi wa Lamadi, mkoani Simiyu, leo Februari 12, 2025, Heche amesema kuwa hali ya maisha ni ngumu kiasi kwamba hata kama kiingilio cha kwenda mbinguni kingekuwa Sh. 20,000, wengi wangekosa fursa hiyo kwa kushindwa kumudu gharama.
Heche amesisitiza kuwa ni wakati wa kufanya siasa za kushinikiza uwajibikaji ili rasilimali za Taifa zitumike kwa maslahi ya Watanzania wote. Aidha, ameeleza kuwa kumekuwa na vilio kutoka kwa vijana wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini, ambapo mara nyingi hujikuta wakibugudhiwa na watu wenye leseni, hali inayowakosesha haki yao ya kunufaika na rasilimali hizo.
Kuhusu sekta ya kilimo, Heche amelalamikia bei ya pamba, akidai kuwa pamoja na ubora wake, bado inanunuliwa kwa Sh. 800 kwa kilo, hali inayowaumiza wakulima. Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa serikali kutumia rasilimali ya Ziwa Victoria ili kuboresha kilimo cha umwagiliaji na kuondoa utegemezi wa mvua kwa wakulima wa mpunga katika Kanda ya Ziwa.
Aidha, amewaomba wananchi wa Lamadi kuungana na CHADEMA kuhakikisha kuwa kila Mtanzania ananufaika na rasilimali za Taifa na kwamba watumishi wa umma wanalipwa stahiki zao ipasavyo.
“Sisi kama wananchi tukiendelea kudhulumiwa, mimi na Tundu Lissu hatutakaa kimya. Tuungeni mkono kwa kutoa hata Sh. 1,000 ili kutuwezesha kusimamia maslahi yenu. Tutakuwa na nguvu zaidi pale mtakapotupa nguvu ya kuwazungumzia,” amesema Heche.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED