ASILIMIA 25 pekee ya wanafunzi waliofanya mtihani wa somo la hisabati, Mtihani wa Taifa Kidato cha Nne Mwaka 2024 nchini, walifaulu mtihani huo, huku asilimia 74.6 wakifeli.
Vilevile matokeo ya somo hilo, kwa mwaka 2023, ni asilimia 25 walifaulu somo na wengine 74.5 wakifanya vibaya.
Hali hiyo imezua wasiwasi miongoni mwa wadau wa elimu nchini, ambao wamesisitiza umuhimu wa walimu kutimiza majukumu yao ipasavyo, ili kuboresha kiwango cha ufaulu.
Mafunzo hayo, yamefanyika katika Shule ya Sekondari ya Ufundi Mtwara, huku akisisitiza kuwa walimu wanapaswa kutumia mbinu bora zitakazosaidia kuongeza kiwango cha ufaulu.
Dk. Mbiling’i ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) Idara ya Sayansi, Hisabati na Teknolojia (STEM), amesema serikali hutumia gharama kubwa kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, kutoa mafunzo kwa walimu wa masomo ya hisabati, ili kuwapatia ujuzi kufundisha somo hilo.
Dk. Mbiling’i amesisitiza kuwa ni muhimu thamani ya fedha inayotolea ilete tija, kwa kupata matokeo mazuri ya mitihani, ili kuona faida ya mafunzo hayo ambayo hutolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, kupitia Mradi wa Kuimarisha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP).
Akifungua mafunzo hayo, Ofisa Elimu Mkoa wa Mtwara, John Lupenza, amesema mafunzo hayo ni fursa kwa walimu kujifunza mbinu mbalimbali za ufundishaji, ambazo zitawasaidia kutimiza majukumu yao kwa ufanisi.
Amemtaka kila mwalimu anayeshiriki mafunzo hayo, kubeba jukumu la kuhakikisha somo analofundisha linafanya vizuri, ili kuwasaidia wanafunzi kufikia ndoto zao na kuwezesha kuzalisha wataalam wenye ujuzi wa aina mbalimbali.
Mratibu wa Mafunzo, Kituo cha Mtwara, Majaliwa Mkalawa, ameeleza kuwa lengo la mafunzo endelevu ya walimu kazini, ni kuwapa mbinu mpya zitakazowasaidia wakati wa kuwasilisha mada ngumu, ambazo wanafunzi wengi hawazielewi au kuziogopa katika masomo ya sayansi na hisabati.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED