Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu amelionya kundi la Hamas kuwa itamaliza usitishaji vita huko Gaza na kuanzisha upya mapigano makali ikiwa kundi hilo halitawarudisha mateka wao ifikapo Jumamosi mchana.
Benjamin Netanyahu amesema ameviamuru vikosi vya Israel kukusanyika ndani na karibu na Gaza kujibu tangazo la Hamas kwamba inaahirisha kuwaachilia mateka zaidi hadi wakati mwingine.
Netanyahu hakutaja iwapo alikuwa anataka kuachiliwa kwa mateka wote 76 waliosalia, au watatu tu wanaopaswa kuachiliwa Jumamosi hii lakini waziri alisema alimaanisha kila mtu.
Hamas ilijibu kwa kusema imesalia na nia ya dhati kwa makubaliano ya kusitisha mapigano na kwamba Israel inawajibika kwa matatizo au ucheleweshaji wowote.
Kundi hilo limeishutumu Israel kwa kukiuka mkataba wa wiki tatu wa kusitisha mapigano, ikiwa ni pamoja na kuzuia misaada muhimu ya kibinadamu madai ambayo Israel imekanusha.
Uamuzi wa Hamas wa kuchelewesha kuachiliwa kwake uliopangwa wikendi hii ulimfanya Rais wa Marekani Donald Trump kupendekeza kuwa Israel ifute makubaliano hayo kabisa isipokuwa iwapo mateka wote watarudishwa ifikapo Jumamosi.
CHANZO:BBC SWAHILI
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED