DC Mapunda: ‘Ardhi imelaaniwa’

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 11:12 AM Jan 26 2025
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria, jijini Dar es Salaam
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Sheria, jijini Dar es Salaam

MKUU wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, amesema ameanza kuamini msemo usemao kwamba, ardhi imelaaniwa kwa sababu kila afaye huenda chini.

Mapunda amesema hayo katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya sheria jijini Dar es Salaam yaliyofanyika viwanja vya Mnazi mmoja, akidai kila panapo kucha kuna dhuluma ya ardhi.

Amewataka wananchi wajitokeze katika viwanja hivyo, ili wapate elimu ya kutosha kuhusu haki madai na mahakama kwa ujumla.

"Kuna msemo unasema ardhi imelaaniwa kwa sababu tukifa tunaenda chini, mimi naanza kuamini hivyo, kwa sababu haiwezekani kila ukiamka asubuhi shughuli ni aridhi, dhuluma ya ardhi. Lakini niwashukuru na kuwapongeza muda wote mmesimamia sheria vizuri.

"Tunatambua mnafanya kazi ya kusimamia taratibu zote katika jamii niwaombe katika wiki hii, muendelee kutoa elimu kwa kila atakayefika hapa, ili jamii yetu iendelee kuwa ya kistaarabu na ijue kwamba mahakama ndiyo kimbilio lao," amesema Mapunda 

Amewata watumishi wa mahakama na na wadau wengine sheria wafanye kazi bila kuchoka kwa kuwa ndio msalaba ambao Mungu amewapatia,  na kwa muda mfupi aliofanya kazi kama Mkuu wa Wilaya, amebaini kazi kubwa ni kutatua migogoro ya ardhi.

Mapunda ametoa rai kwa wananchi kujitokeza, kwa ajili ya kujifunza kuhusu utendaji kazi wa mahakama na mifumo mengine ya kisheria, watajua haki zao mahakamani na mifumo ya utoaji haki.

"Niwaombe wananchi wa Dar es Salaam, mfike hapa viwanja vya Mnazi Mmoja, ni mara chache sana huduma hizi kuzipata bure," amesema Mapunda 

Pia, amesema kuwa mifumo ya utoaji haki imeimarika kiasi kwamba, mahakimu au majaji wanaweza kusikiliza kesi kutokea sehemu yoyote ya nchi kwa njia ya kidigatali. 

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salam, Jaji Salima Maghimbi amesema Novemba 6, 2023, ilikuwa siku ya kihostoria ya mahakama kuhama kutoka kwenye mifumo ya analogia kwenda kidigatali.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Jaji Salima Maghimbi, akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria, jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa mageuzi hayo yamesababisha mafanikio katika mahakama na mwaka 2024 mashauri 37,988 yalisajiliwa na kati ya hayo 37,953 yalisikilizwa.

Pia mfumo ulisaidia kufikia kiwango cha kuondoshwa kwa asilimia 100 na hadi Desemba, 2024 mashauri 7, 343 sawa na asilimia nane ya mashauri yaliyobaki.

"Tuliweza kuondoa mrundikano wa mashauri kwa asilimia 80 kutokana na kasi ya kusikiliza mashauri, kwa njia ya kidigitali," amesema Jaji Maghimbi 

Amesema katika kuadhimisha Wiki ya Sheria nchini,  kutakuwa na mijadala itakayojadili kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu, 'Tanzania ya mwaka 2050 nafasi ya Taasisi zinazosimamia haki madai'.

Pia, amesema mahakama imejipanga kutekeleza kwa vitendo mpango wa Dira yaTaifa wa 2050.

Jaji Maghimbi amesema mahakama itatoa taarifa ya utendaji kazi wake wa mipango yake mkakati inayotekelezwa kwa miaka mitano.

Amesema kuwa katika maadhimisho hayo kutakuwa na uzinduzi rasmi wa Mahakama ya Mwanzo ya Wazo Hill, Januari 31, 2025.