Kikwete aonya wanaotumia kivuli cha dini kujenga chuki

By Ida Mushi , Nipashe
Published at 10:37 AM Jan 27 2025
Kikwete aonya wanaotumia   kivuli cha dini kujenga chuki.
Picha: Mtandao
Kikwete aonya wanaotumia kivuli cha dini kujenga chuki.

RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amewaonya watanzania kuacha kutumia mwamvuli wa dini kujenga chuki na kuleta mifarakano katika jami, hali inayochochea machafuko na uvunjifu wa amani.

Kikwete ambaye ni mwasisi wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), alisema hayo mjini Morogoro mwishoni mwa wiki wakati wa kikao cha kamati, akiwaasa viongozi wa dini kusimama imara kuhakikisha Tanzania inaendelea kubaki kuwa kisiwa cha  amani, utulivu na umoja.

Alisema amani na utulivu kamwe haviwezi kununuliwa dukani badala yake ni lazima watanzania waendelee kuimarisha undugu na mshikamano na kuepuka kubaguana kwa misingi yoyote, ikiwamo ya kiimani, rangi na kabila.

Alitolea mfano chachu ya kushauri uanzishaji taasisi hiyo enzi za serikali aliyoongoza kuwa kulisababishwa na mgogoro wa kidini ulioibuka wa kuchinja kati ya waumini wa Kiislam na Kikristo ambapo licha ya kuanzia eneo dogo la Katoro, watu waliusambaza na kuuchochea kuwa wa kiimani na kuleta machafuko, mauaji, majeruhi na uharibifu wa mali.

"Hali ilikuwa mbaya, kila mmoja akachukua upande wake. Ikabidi tuanze kuwadhibiti watu na hata vyombo vya habari vilivyoonekana kuchochea mgogoro na ndio kama alivyosema Sheikh Alhad (Sheikh Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania) tukaitisha mkutano mkubwa sana kuwahi kutokea kwa kuwashiriaha viongozi wa dini zote, wakala na kulala pamoja ili kila mmoja amzoee mwenzake na ukawa mwanzo wa kuanzisha chombo hiki," alisema Rais mstaafu huyo.

Kikwete alielekeza taasisi hiyo kuendelea kusimamia amani, maadili na utulivu na kusaidia utatuzi wa changamoto ya  migogoro ya wakulima na wafugaji na kukiri tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo mwaka 2015 migogoro hiyo imepungua.

Aliwataka waongeze nguvu ili vijana wa Tanzania waishi katika mila na desturi za Tanzania na kuondokana na changamoto ya uvunjifu wa amani, kwa kuwa bado kuna changamoto kwenye malezi, hivyo wasimamie ili vijana wasiharibiwe na utandawazi.

Alikemea baadhi ya vyombo vya habari vinavyotumika kuchochea uvunjifu wa amani, akionya kuwa havitavumiliwa.

Mwenyekiti wa JMAT, Sheikh Alhad Mussa Salum alisema taasisi hiyo haina lengo la kufanya ibada za dini mseto na si chombo cha dini kama baadhi ya watu wanavyofikiria.

Alisema kinachofanyika ni kuwaunganisha viongozi wa dini pamoja na kutafuta amani na utulivu wa nchi huku kila dini ikiendelea kuabudu kwa imani yake na kila mmoja anafahamu imani yake na kuiishi.

Sheikh Alhad pia aliwahimiza viongozi wa dini kufanya matendo mema kwa kuwa wao wanafananishwa na chumvi ambayo ni kiungo muhimu katika mboga. Ikichafuka, haiwezi kusafishwa na kitu chochote. 

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima alisema mkoa huo miaka ya zamani ulikuwa unasifika kwa migogoro ya ardhi na wakulima na wafugaji. Tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo, sifa hiyo inatoweka.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini JMAT, Azim Dewji alisema jukumu la kulinda amani ni la kila mmoja na hata vyama vya siasa ni vyema vikalinda hilo na kufanya siasa ya staha kwa sababu Tanzania ni ya wananchi wote.