Nyuki wavamia shuleni na kujeruhi wanafunzi, walimu

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 10:50 AM Jan 27 2025
Nyuki.
Picha: Mtandao
Nyuki.

WANAFUNZI 27 na walimu wawili wa Shule ya Msingi Sayuni, wilayani Manyoni, mkoa wa Singida wamejeruhiwa na kulazwa hospitalini baada ya kundi la nyuki kuwavamia na kuwashambulia.

Mwalimu wa shule hiyo, Neema  Ng'aa, akizungumza juzi baada ya Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Dk.Vicent Mashinji kutembelea shule hiyo, alisema tukio hilo lilitokea juzi wakati wanafunzi hao wakiwa darasani.

"Nyuki walipovamia shuleni, wanafunzi walianza kukimbia ovyo kujiokoa na walimu waliokwenda kuwasaidia wanafunzi, nao walishambuliwa na kujeruhiwa," alisema.

Mwalimu Bless Mwarabu alisema kuwa baada ya nyuki kuvamia shuleni, ilipigwa kengele, hali iliyosababisha nyuki kuongeza kasi ya kushambulia wanafunzi na kuwajeruhi.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, Dk. Lucy Deo, alisema kuwa baada ya kupata taarifa za tukio hilo, walipeleka magari matatu ya kubeba wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya kuwachukua majeruhi na kuwafikisha hospitalini kwa ajili ya matibabu.

"Majeruhi tuliowachukua ni 27 ambao ni wanafunzi na walimu wawili, tuliwapa matibabu na baadhi yao waliruhusiwa na wengine bado wanaendelea na matibabu," alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Dk. Mashinji, ambaye alifika katika shule hiyo, alielekeza watendaji wote sehemu zinazotoa huduma kwa jamii, wadudu na wanyama hatarishi wadhibitiwe.

"Nielekeze shule zote nikikuta nyuki shuleni, mimi ninaanza na mwalimu wa mazingira na baadaye mwalimu mkuu, maana nyuki kuweka makazi yao shuleni wakati hawasomi wala hakuna kozi ya nyuki, kuna haja gani ya kuwa nao mazingira ya shule," alionya.

Makundi ya nyuki yamekuwa yakiweka makazi kwenye madarasa ya shule na nyumba za ibada mkoani Singida na kusababisha wananchi kushambuliwa.