Kenya yaibana DRC kulipa fidia uvamizi, DRC yaridhia kulipa

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:48 PM Jan 28 2025
Kenya yaibana DRC kulipa fidia uvamizi, DRC yaridhia kulipa.
Picha:Mtandao
Kenya yaibana DRC kulipa fidia uvamizi, DRC yaridhia kulipa.

JAMHURI ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imesema itailipa fidia Kenya kutokana na uharibifu uliofanywa katika ubalozi wake, Mjini Kinshasa baada ya wenyeji kushambulia na kupora mali zake mapema hii leo Januari 28, 2025, huku waasi wa M23 wakiendelea kukaribia Mji mkuu.

Awali akieleza kusikitishwa na uvamizi huo, Katibu Mkuu wa Baraza la Mawazi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, amelaumu shambulio hilo, akisisitiza kwamba amewasiliana na mwenzake katika Wizara ya Mambo ya Nje ya DRC kujadili suluhisho zinazowezekana.

"Kenya ina wasiwasi mkubwa kuhusu mashambulizi dhidi ya ofisi za ubalozi wetu na wafanyakazi huko Kinshasa, DRC na umati wa watu waliokuwa wakipinga mzozo wa vurugu katika Mashariki ya DRC. Mashambulizi yasiyo ya lazima, kupora, na uharibifu wa mali pia umelenga ubalozi wa Uganda. Kulikuwa na mipango ya waandamanaji kushambulia na kufanya shambulio dhidi ya ubalozi wa Afrika Kusini, Marekani, na Ubelgiji," amesema Mudavadi.

Aidha Musalia Mudavadi amesema sakata hilo limejibiwa haraka na Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri na Waziri wa Mambo ya na Masuala ya Diaspora wa DRC, Thérèse Kayikwamba Wagner, ambaye amekiri tukio hilo la kusikitisha na kuthibitisha kwamba hatua za haraka zinachukuliwa ili kushughulikia hali hiyo na kurejesha utawala.

Mudavadi amesema imebidi aweke wazi kwa Wagner kwamba vitendo kama hivyo ni ukiukaji wa makubaliano ya kimataifa, na kwamba mamlaka ya DRC lazima ihakikishe usalama wa wafanyakazi wa kidiplomasia kulingana na sheria za kimataifa, hasa Mkataba wa Vienna kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia.

Mkataba huo unahitaji nchi zinazokaribisha mabalozi kuchukua hatua zote zinazofaa kulinda majengo ya ujumbe dhidi ya uvunjaji au uharibifu, kuzuia machafuko yanayoweza kuathiri amani au heshima yake na kuhakikisha usalama, uhuru na heshima ya wafanyakazi wa kidiplomasia kwa kuzuia mashambulizi yoyote dhidi yao.

"Shambulio la kikatili, kupora, na uharibifu wa mali ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na kanuni na taratibu za muda mrefu za Mkataba wa Vienna kuhusu Mahusiano ya Kidiplomasia, hasa Kifungu 22 (2) na Kifungu 29 ambacho kinaeleza wazi kwamba majengo ya ujumbe na mtu au wakala wa kidiplomasia hayawezi kuingiliwa," amesema Mudavadi.

Amedai shambulio hilo kuwa limetokea mbele ya maofisa wa usalama wa DRC ambao hawakuchukua hatua yoyote ya kupunguza hali hiyo. 
Kadhalika amesema baada ya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa DRC amekiri na kuahidi kuwa serikali itafanya tahimini kuilipa serikali ya Kenya fidia kwa uharibifu uliojitokeza katika  ubalozi huo.