Balozi za Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi, Marekani nazo zashambuliwa na waandaaji, EU yalaani

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 11:31 AM Jan 29 2025
Balozi za Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi, Marekani nazo zashambuliwa na waandaaji, EU yalaani.
Picha: Mtandao
Balozi za Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi, Marekani nazo zashambuliwa na waandaaji, EU yalaani.

KATIKA mfululizo wa uvamizi wa balozi za nje zilizopo nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), balozi za Ufaransa, Ujerumani, Ubelgiji, Uholanzi na Marekani zimevamiwa na kufanyiwa vurugu na waandamanaji wa ndani wakishinikiza kudhibitiwa kwa mapigano mjini Goma.

Uvamizi wa balozi hizo uliofanyika Januari 28, muda mfupi baada ya vurugu za namna hiyo kufanyika katika ubalozi wa Kenya na Uganda, unalenga kuzishinikiza jumuiya ya kimataifa iishtaki Rwanda kwa kuhusika kwake katika mzozo huo.

Sauti mbalimbali za waandamanaji hao zilisikika zikisema, "Tunakanusha unafiki wa jumuiya ya kimataifa," na "Lazima wawambie Rwanda ikome na huu uvamizi."

Baadhi ya waandamanaji pia wanadai kuwa mataifa ya kigeni yana ushirika katika uvamizi huu, ambao serikali ya Kongo inasema pia unajumuisha wanajeshi wa Rwanda.

Msemaji wa Wizara ya Maendeleo ya Ujerumani alisema Jumanne kwamba wamefutilia mbali mashauriano ya serikali yaliyopangwa kufanyika Februari na Rwanda na wanashirikiana na jumuiya ya kimataifa kutafuta suluhisho la mgogoro huu.

Shirika la Umoja wa Ulaya (EU) limelaani uvamizi wa balozi za kigeni unaofanywa na wazawa katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Msemaji Mkuu wa Masuala ya Kigeni wa EU, Kaja Kallas, alisema jioni ya jana mjini Brussels kwamba balozi zinatakiwa kulindwa kwa misingi ya kidiplomasia kulingana na Mkataba wa Vienna kuhusu Mambo ya Kidiplomasia.

Ufaransa limekuwa taifa la pili kukemea uvamizi huo, likitanguliwa na Kenya, juu ya uvamizi unaotajwa kuharibu rasilimali za mataifa ya kigeni katika balozi zake.

Ujerumani imesema imefuta mipango ya mashauriano na Rwanda kutokana na tuhuma za kuunga mkono waasi wa M23, ambao uvamizi wao umeanzisha ghasia hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot, alikemea vikali uvamizi wa balozi ya Ufaransa katika mji mkuu, Kinshasa.

"Mashambulizi haya hayakubaliki. Kila kitu kinafanyika kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wetu na raia wetu," alisema Barrot.

Balozi za Ubelgiji, Uholanzi, Kenya, Rwanda, Uganda, na Marekani pia zimekumbwa na uvamizi wa waandamanaji wakati mamia ya maelfu ya watu wakikimbia mapigano mashariki mwa nchi hiyo.

Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi wakati waandamanaji walipokuwa wakipita mbele ya balozi hizo, wakivunja au kuwasha moto sehemu za majengo ya kidiplomasia.

Waziri wa Mawasiliano wa DRC, Patrick Muyaya, alisema polisi wamepata udhibiti wa mji mkuu, Kinshasa, na wameimarisha usalama katika balozi.

Waandamanaji wanafanya maandamano dhidi ya kuendelea kwa waasi wa M23 walioungwa mkono na Rwanda kuingia Goma, mji mkubwa mashariki mwa DRC ambako mzozo unaendelea.