Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Kitaifa la Afrika Kusini (SANDF), Jenerali Rudzani Maphwanya, amejibu kauli ya Rais wa Rwanda, Paul Kagame, kuhusu mchango wa vikosi vya ulinzi wa amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), akisisitiza kuwa jeshi la kikanda limeisababishia hasara kubwa M23 katika mapambano ya hivi karibuni.
Jenerali Maphwanya amesema kuwa Kikosi cha Kulinda Amani cha Kikanda nchini DRC (SAMIDRC), kinachojumuisha vikosi vya jeshi kutoka Afrika Kusini, Malawi, na Tanzania, kimefanikiwa kuwadhibiti waasi wa M23, ambao wamekuwa wakisababisha machafuko mashariki mwa nchi hiyo.
Katika taarifa yake leo, Maphwanya alieleza kuwa waasi wa M23 wanadaiwa kupata mafunzo na kuungwa mkono na Serikali ya Rwanda, ambayo ni jirani wa DRC.
"Tishio kuu katika eneo hili linatokana na kundi la waasi ambalo linadaiwa kuwa na silaha, kuungwa mkono, kufunzwa, na kusaidiwa na Jeshi la Ulinzi la Rwanda. Katika majibizano ya hivi karibuni, vikosi vyetu vya SAMIDRC vilifanikiwa kupambana na M23 na kuwazuia kutekeleza malengo yao ya kusonga mbele hadi Goma," alisema Maphwanya.
Alifafanua kuwa Januari 23, 2025, waasi wa M23 walifanya shambulio kubwa wakijaribu kuteka mji wa Sake, ili kufanikisha mpango wao wa kufikia mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini, Goma.
"Katika mapambano hayo makali, askari wetu walionyesha ujasiri mkubwa na kufanikiwa kuwazuia waasi wa M23 kusonga mbele. Hata hivyo, tulipoteza wanajeshi 13 wa Afrika Kusini katika mapigano hayo," alisema Maphwanya.
Akaongeza kuwa Januari 27, 2025, kambi ya SANDF ilishambuliwa kwa mabomu ya masafa marefu, na kusababisha vifo vya wanajeshi wengine watatu wa Afrika Kusini.
Akijibu kauli ya Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais Paul Kagame alisema kuwa Afrika Kusini haina nafasi ya kuwa mpatanishi wa amani katika mgogoro wa DRC.
"Ikiwa Afrika Kusini inataka kusaidia kutafuta suluhu za amani, hilo ni jambo jema, lakini hawana nafasi ya kuwa wapatanishi au kusimamia mchakato wa amani. Na ikiwa watachagua makabiliano, Rwanda ipo tayari kushughulikia suala hilo siku yoyote," alisema Kagame kupitia mtandao wake wa X (zamani Twitter).
Kwa upande wake, Jenerali Maphwanya alisisitiza kuwa SAMIDRC inasalia imara katika juhudi za kurejesha amani mashariki mwa DRC, huku ikitafuta suluhisho la kudumu kwa mgogoro huo.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mbali na wanajeshi 13 wa Afrika Kusini waliouawa, wanajeshi watatu wa Malawi waliokuwa sehemu ya ujumbe wa SAMIDRC pia waliuawa katika mashambulizi ya M23.
Aidha, mwanajeshi mmoja kutoka Uruguay, aliyekuwa sehemu ya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu nchini DRC (MONUSCO), alifariki dunia katika vita dhidi ya waasi wa M23.
Serikali ya DRC, Umoja wa Mataifa, na Marekani zimeeleza kuwa kundi la M23, linaloongozwa na watu wa kabila la Watutsi, linaungwa mkono na Rwanda kwa lengo la kulinda maslahi ya Watutsi walioko mashariki mwa DRC.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED