‘Kampeni ya Samia haitawaacha salama kisheria wakiukaji haki’

By Godfrey Mushi ,, Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 09:55 AM Jan 30 2025
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro (wa tatu kushoto), akipata maelezo kabla ya kuzindua Kampeni ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro jana.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro (wa tatu kushoto), akipata maelezo kabla ya kuzindua Kampeni ya Msaada wa Sheria ya Mama Samia, mjini Moshi, mkoani Kilimanjaro jana.

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, amesema Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia itapita kila halmashauri, wilaya, kata, vijiji na vitongoji na mitaa yote kuhakikisha kila mtanzania ananufaika na huduma hiyo bila malipo.

Aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa kampeni hiyo kwa mkoa wa Kilimanjaro, viongozi mbalimbali wakishiriki uzinduzi huo.

"Kwenye kampeni hii, hakuna jiwe litakaloachwa bila kuguswa. Kila mgogoro utatatuliwa. Tuna awamu ya kwanza na ya pili, hivyo kila Mtanzania mwenye mgogoro wake ataguswa na wale waliozoea kukiuka haki za watu, hatutawaacha salama, maana tutapita kila kona.

"Katika mikoa 16 tuliyopita, tumeona wananchi wengi wana kiu ya haki na ndiyo maana wamekuwa wanajitokeza kwenye kampeni na sisi tunawatimizia mahitaji yao, Haya ni maono na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyeona kiu ya haki ya watanzania," alisema.

Dk. Ndumbaro alisema kampeni hiyo yenye maudhui ya kusaidia wananchi, ina mambo 10 na itapita kila eneo la Tanzania Bara na Visiwani.

"Katika kampeni hii kila kichaka kitakatwa na kuchomwa moto, kuna watu wanajificha kwenye vichaka vya ukatili tutavikata ili haki itendeke. Mama Samia Legal Aid ni ibada kwa sababu inatenda jambo jema lililoandikwa na maandiko yote.

"Tutahakikisha Mama Samia Legal Aid inaleta haki itakayoinua taifa la Tanzania, kampeni hii ni jambo la kikatiba na sheria na imekuja na falsafa ya 'Gusa Achia Twende na Mama Samia Legal Aid' na pia imekuja na falsafa ya 'Ubaya Ubwela' kwa wanaokiuka haki za binadamu, wanaokiuka sheria, wanaofanya ukatili wa kijinsia tutawanyoosha," alisema.

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Boniface Mwabukusi, alisema huduma ya msaada wa kisheria kwa wananchi ni kama ibada, hivyo ni wajibu wa wanaotoa huduma hiyo kuifanya kwa unyenyekevu na kwa ukamilifu.

Alisema migogoro mingi iko kwenye mirathi na ardhi na kwamba hayo yote yanachangiwa na watu kuogopa kuandika wosia, hali ambayo imekuwa inachochea migogoro baada ya mhusika kufariki dunia.

"TLS section IV inataja huduma hii ya msaada wa sheria na tunaipa huduma hii kipaumbele kikubwa sana kusukuma huduma za msaada wa kisheria kwa wananchi. Tutaunga mkono serikali kuwasaidia wananchi wengi wenye shida wapate haki," alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdini Babu alipongeza kampeni hiyo kupelekwa mkoani mwake, akidokeza kuwa wapo wananchi wengi wenye changamoto ya migogoro ya kisheria, lakini hawajui sehemu ya kwenda kupata haki.

"Tuna madawati ya msaada wa sheria kwenye ofisi mbalimbali hapa mkoani, lakini baada ya kuzindua leo (jana) hapa tutakwenda kwenye kata zote ambako kuna wananchi wengi wenye changamoto ya kupata haki. Kwa hiyo kampeni hii ni mwafaka," alisema.

Mwakilishi wa Chama cha Mawakili wa Serikali, Yohana Marko, alisema mawakili wa serikali wana wajibu wa kisheria wa kutoa elimu ya msaada wa kisheria huku akiahidi kuwa chama kitatekeleza kwa nguvu zote suala la msaada kwa kufuata mwongozo wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Alisema hiyo itakuwa ajenda ya kudumu ndani ya Chama cha Mawakili wa Serikali na uongozi wa chama utahakikisha wananchi wanaendelea kunufaika na huduma za msaada wa sheria.

"Ninakupongeza waziri kwa kutenga muda wako na ninakuhakikishia kampeni hii itatoa matokeo chanya kwa kutatua migogoro ya mirathi, ardhi na migogoro ya ndoa ambayo ndiyo imekuwa inasumbua kwenye jamii. Ninatoa wito kwa mawakili wa serikali kushiriki kikamilifu," alisema.

Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Jacob Tarimo alisema watu wengi wamekuwa wanafika ofisini kwake kuomba msaada wa sheria, hivyo ujio wa kampeni hiyo ni ukombozi kwao.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Amon Mpanju alimpongeza Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Ndumbaro, kwa kufanikisha huduma hiyo ya msaada wa sheria kwa wananchi wasio na uwezo kupata haki zao.

*Imeandaliwa na Godfrey Moshi na Joseph Mwendapole