DSE yarahisisha ununuzi wa hisa kupitia mtandao wa simu

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 05:05 PM Jan 30 2025
DSE yarahisisha ununuzi wa hisa kupitia mtandao wa simu.
Picha: Mtandao
DSE yarahisisha ununuzi wa hisa kupitia mtandao wa simu.

Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeanzisha huduma mpya inayowawezesha wananchi kununua na kuuza hisa kwa njia ya mtandao wa simu, hatua inayotarajiwa kuongeza ushiriki wa wananchi katika uwekezaji na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Peter Nalitolela, alisema huduma hiyo inalenga kuwarahisishia wananchi mchakato wa kununua na kuuza hisa bila vizuizi vya muda na mahali.

"Zamani, watu walilazimika kusubiri hadi saa nne asubuhi wakati soko linafunguliwa ili kufanya miamala ya hisa. Lakini sasa, kupitia huduma hii mpya, mtu anaweza kununua au kuuza hisa wakati wowote na kutoka mahali popote," alisema Nalitolela.

Aliongeza kuwa hatua hiyo itaongeza ushiriki wa wananchi katika soko la hisa, kuwawezesha kuwekeza kwa urahisi na kujiandaa kwa maisha ya baadaye.

1

Kwa upande wake, Kaimu Ofisa Mkuu wa Yas, Innocent Rwetabura, alisema wameingia makubaliano na DSE ili kufungua fursa zaidi za uwekezaji kwa Watanzania kupitia mfumo huu wa kidijitali.

"Lengo letu ni kuhakikisha Watanzania wote wanapata nafasi ya kuuza na kununua hisa muda wowote, ndani na nje ya nchi, kwa urahisi kupitia simu zao," alisema Rwetabura.

Huduma hii mpya inatarajiwa kuvutia wawekezaji wapya, kuongeza uwazi wa soko, na kusaidia ukuaji wa uchumi kupitia ushiriki mpana wa wananchi katika uwekezaji wa hisa.

2